TAASISI ya Tanzania Youth Elite Community (TYEC),imemtunuku Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu cheti cha heshima kama ishara ya kutambua uzalendo wake halisi na juhudi zake katika kuchagiza maendeleo kwa wananchi wake.
Cheti hicho cha heshima amekabidhiwa Disemba 22,2022, na Katibu Mkuu wa TYEC Nghwigulu Shigela wilayani Ikungi Mkoani Singida.
“Tunakupa cheti hiki ili kuonyesha namna tunavyoguswa na utumishi wako jimboni,umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo,tunajua kiu na dhamira yako uliyonayo inakusukuma kufanya hivi,tunakuombea na tupo nyuma yako,”alisema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa cheti hicho,Mtaturu amesisitiza kuwa tuzo hiyo ni heshima kwa wananchi wote wa Wilaya ya Ikungi.
“Niwashukuru ndugu zangu TYEC kwa kuona na kutambua juhudi zangu,wakati naomba kura niliahidi kuwatumikia wana Singida Mashariki na dhamira hii nitaendelea kuitekeleza kwa vitendo ili kubeba imani waliyoionyesha kwangu,”ameshukuru.
Mtaturu amesema tuzo hiyo ni chachu kwao katika kuongeza bidii ya kupaza sauti kuisemea jamii yenye uhitaji.
“Ninapopokea tuzo hii namshukuru Mungu kwa kutupa vipawa na karama mbalimbali zinazotupa uwezo wa kuchambua na kuzitafuta fursa kwa faida ya jamii yetu,”amesema.
Amemshukuru sana mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapelekea fedha zinazotekeleza miradi lukuki kwenye maeneo yao na hivyo kuondoa kero katika sekta ya Elimu, Afya,Miundombinu ya Umeme, Maji na Barabara.