Na Dotto Mwaibale, Singida
ZAIDI ya Sh.67 Milioni zimeelekezwa kuchagiza na kuchochea miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Singida Mashariki. Akizungumza Disemba 22,2022 wakati akiongoza kikao cha kamati ya mfuko wa Jimbo, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu alisema fedha hizo zinakwenda kutekeleza miradi mbalimbali kwenye jimbo hilo na akaomba zikatumike kukamilisha miradi yenye viwango na thamani halisi ya fedha hizo. Katika hatua nyingine Taasisi ya Tanzania Youth Elite Community (TYEC) kwa kuutambua uzalendo halisi wa nchi imemtunuku tuzo ya heshima mbunge huyo ikiwa ni kutambua juhudi zake katika kuchagiza maendeleo ya wananchi jimboni humo. Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo Shigela Denis alisema wameamua kumtunuku tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa anaoufanya wa kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo. “Mbunge Mtaturu amekuwa ni chachu kubwa ya maendeleo katika jimbo la Singida Mashariki na kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa katika jimbo hilo amefanya mambo makubwa na kwa kulitambua hilo kupitia taasisi yetu tumeamua kumtunuku tuzo hii ya heshima” alisema Shigela, Akizungumza baada ya kutunukiwa tuzo hiyo aliishukuru taasisi kwa kutambua mchango wake na kueleza tuzo hiyo ni ya Heshima kwa wananchi wote wa Wilaya ya Ikungi na si peke yake. |