*******************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Disemba 22
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kushirikiana na Shirika la kusaidia watoto Duniani (UNICEF) umetoa msaada wa vifaa vya usafi 16,754 ambavyo vinatarajia kugawiwa kwa watoto wa kike waliobalehe waliopo kwenye mfuko huo katika Halmashauri Tisa zilizopo mkoani humo.
Vifaa hivyo ni kwa ajili ya usafi ikiwemo sabuni ,ndoo pamoja na taulo za kike.
Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Pwani,Roselyn Kimaro alieleza lengo ni kufikia watoto hao 16,754 ambapo hadi sasa wameshagawiwa watoto 11,350 na zoezi linaendelea.
Hata hivyo ,aliwataka walengwa hao kutumia vizuri misaada wanayopewa ili kuwasaidia na kuwataka wazazi kuzungumza na watoto wao hasa kipindi wanachobalehe kwa Lengo la kuwa wasafi,kujiepusha na mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa.
Roselyn aliwasihi watoto hao kuacha kuchangia taulo zao za kike ili kujiepusha na magonjwa .
Nae Mratibu wa Tasaf Chalinze Flora Godfrey Barakana alisema lengo la msaada huo ni kumsaidia mtoto wa kike awe huru hasa katika kipindi cha kupata hedhi yake ya mwezi.
Kwa upande wake Anita Philemon mratibu wa Tasaf Kibaha Mjini alisema vifaa hivyo vitasaidia watoto hao kwa Maendeleo yao shuleni na watapewa mafunzo ya namna ya kutumia kabla ya kuvitumia na kuwaomba taulo za kike ni kwa ajili ya msichana mmoja mmoja na sio vya kuazimana ili kulinda afya zao.
Mnufaika wa Tasaf ,Sadi Athumani alieleza elimu waliyoipata wataenda kuifanyia kazi na kuwa mabalozi kwa wengine kuwafundisha kujenga tabia ya usafi na kujilinda na vishawishi ili kuendelea na masomo kutimiza ndoto yao .