Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Viongozi mbalimbali alipowasili Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Desemba, 2022 kwa ajili ya kushiriki katika Shughuli ya Kufunga Njia ya Kuchepusha Maji na Kuanza Ujazaji wa Maji kwenye Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye Mto Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Desemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme (Megawati 2115) la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye Mto Rufiji Mkoani Pwani tarehe 22 Desemba, 2022.
*********************
Na. Seleman Msuya, Rufiji
SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kasi ya utekelezaji wa miradi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inamfanya amuone anafanya zaidi.
Dk Tulia amesema hayo leo wakati akizungumza mbele ya Rais Samia kwenye hafla ya zoezi la ujazaji maji katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), iliyofanyika Rufiji mkoani Pwani.
Spika Tulia amesema baada ya kupita na kuangalia shughuli zilizofanyika ametambua kuwa kazi kubwa imefanyika kwa kipindi kifupi cha Rais Samia.
“Mimi nadiriki kusema Rais Samia umefanya, unafanya na kuzidi kwani mradi huu umefikia sehemu nzuri ya kupongezwa,”amesema.
Amesema mradi huo kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 70 hivyo ni matumaini yake utaisha katika muda uliopangwa.
Dk Tulia amesema yeye kama kiongozi wa Muhimili wa Bunge atahakikisha unazungumziwa vizuri ndani na nje ya Bunge.
“Bunge litaendelea kuunga mkono miradi yote ambayo inatekelezwa nchini, ukiwemo huu wa JNHPP ambao unaenda kukuza uchumi wetu siku zijazo,”amesema.
Spika Tulia amesema ni imani yake mradi huo utaenda kugusa sekta zingine na nchini kwa ujumla.