Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema
akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa katika shule
za sekondari Manispaa ya Songea ambapo serikali imetoa shilingi
bilioni 1.5 kujenga madarasa 76 ambayo yamekamilika
baadhi ya madaarsa katika Halmashauri ya
Manispaa ya Songea ambayo yamekamilika na yanatarajia kuanza kuchukua
wanafunzi Januari 2023
MWENYE Suti ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa
Pololet Mgema akiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama kukagua mradi wa
madarasa katika Manipaa ya Songea
……………………………
Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mheshimiwa Pololet Mgema amesema Halmashauri tatu katika Wilaya ya Songea zimekamilisha kwa mafanikio makubwa kazi ya kujenga madarasa 96 ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mgema amesema hayo baada ya kukagua madarasa 29 kati ya 76 yaliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
“Sisi Wilaya ya Songea tumekwishafanya kazi tuliotumwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tumeikamilisha kwa mafanikio makubwa “,alisema
na kuongeza kuwa wanafunzi wote watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 watapata mahali pazuri pa kusomea.
Amesema madarasa yote 96 yaliyojengwa Wilaya ya Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9 yamejengwa katika viwango na ubora wa hali ya juu.
Amebainisha zaidi kuwa madarasa yote yamewekewa malumalu,nishati ya umeme,viti na meza pamoja na milango yenye viwango bora inayolingana na thamani ya madarasa.
Amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuleta fedha shilingi bilioni 1.9 katika Wilaya ya Songea ambazo zimejenga madarasa 76 katika Manispaa ya Songea kwa shilingi bilioni 1.5,madarasa kumi katika Halmashauri ya Madaba ambayo yamegharimu sh milioni 200 na madarasa kumi katika Halmashauri ya Songea ambayo yamegharimu shilingi milioni 200.
Hata hivyo amesema kazi ya ujenzi wa madarasa iliyofanywa katika Wilaya ya Songea inakwenda kujenga taswira katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kwa sababu asilimia 80 ya madarasa yote yaliyopewa fedha za madarasa yapo Wilaya ya Songea.
Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Songea wakiwemo Monica Haule na Frank Komba wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea kero ya vyumba vya madarasa wanafunzi wa shule za sekondari.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Ruvuma imetoa shilingi bilioni 3.2 kujenga madarasa 156 katika shule za sekondari ili kukabiliana na upungufu wa madarasa kwa wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza Januari 2023.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma