Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kimempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo jimboni pamoja na kushinda nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu taifa kupitia uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni kwa kujaza nafasi mbalimbali ngazi ya taifa
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Mhe Yusuph Bujiku wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kukagua uhai wa chama na kuhamasisha ujenzi wa ofisi za chama hicho kwa ngazi ya matawi na kata ambapo akiwa kata za Kahama na Nyamhongolo amekemea makundi ndani ya chama pamoja na kuhakikisha Serikali inasimamiwa vizuri
‘.. Katika uchaguzi uliokwisha Ilemela tuna la kujivunia, Tumepata mjumbe wa halmashauri kuu taifa(mnec) kutoka ndani ya wilaya yetu, tumpongeze na tujivunie ..’ Alisema
Aidha Mhe Bujiku amewataka viongozi waliochaguliwa hivi karibuni kwa ngazi ya matawi na kata kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na kwamba hatavumilia kiongozi yeyote asiyetimiza wajibu wake ikiwemo kufanya ziara za kukagua utekelezaji wa Ilani na uimarishaji wa chama
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM kata ya Kahama Mathayo Nocholaus amemuahidi mwenyekiti huyo wa wilaya kuwa katika kipindi chake hataacha kuisimamia Serikali kuhakikisha kilichoahidiwa na chama kwa wananchi kwa kipindi cha miaka mitano kinatekelezwa na kwamba watendaji wavivu hawana nafasi ndani ya kata hiyo
Luhela George ni katibu wa CCM kata ya Kahama ambapo amefafanua kuwa katika jitihada za ujenzi wa ofisi za matawi na kata wanachama wa CCM kata ya Kahama mpaka sasa wameshachangia zaidi ya kiasi cha shilingi laki tatu na elfu arobaini na tatu huku zoezi hilo likiendelea kuhakikisha ofisi zinajengwa kila tawi na kata
Farida Joachim ni miongoni mwa wanachama wa CCM kata ya Kahama ambapo yeye ameipongeza kamati ya siasa ya wilaya hiyo kwa kuamua kufanya ziara ngazi za matawi na kata ili kukiimarisha chama hicho na kutoa morali kwa viongozi wengine waweze kutimiza wajibu wao sambamba na kuomba ziara hizo ziendelee kuwa endelevu