Na. A/INSP FRANK LUKWARO
Imeelezwa kuwa kufunguliwa kwa Ofisi mpya za Dawati la Jinsia na Watoto katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara kutasaidia kupunguza vitendo vya ukatili ikiwemo vya ukeketaji kwa Watoto wa kike ambayo vipo katika Wilaya hiyo.
Hayo yamesemwa na Wakazi wa Kiteto wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto zilizojengwa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya uzazi (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la Utu wa Mtoto (CDF).
Bw.Lomnyaki Mkulati, Salumu Khatib na Zuberi Mtambo wakazi wa Kiteto wamesema uwepo wa Dawati hilo utatoa fursa kwa Watu wanaofanyiwa ukatili hususani Watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukeketaji ambavyo vipo katika Wilaya hiyo kutokana na mil ana desturi za makabila yaliyopo katika maeneo hayo.
Pia wamesema wanaume nao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili lakini wamekuwa wakiona aibu kutoa taarifa jambo ambalo limekuwa likiongeza kuwepo kwa vitendo hivyo.
Mapema akifungua Dawati hilo Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mbaraka Al Haji Batenga amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa Wanaofanya vitendo hivyo wanaadhibiwa na kuwataka Wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa dawati hilo kutoa taarifa ambazo zitawezesha kukamatwa kwa wanaofanya vitendo hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Maria Nzuki amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na Wadau katika kujenga madawati mikoa mbalimbali nchini ili kurahisha upatikanaji wab huduma.