*******************
NA FARIDA MANGUBE. MOROGORO
MWEKEZAJI katika kijiji cha Merela Kata ya Chita katika halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Mkoani Morogoro ameshindwa kuendelea na shughuli za uwekezaji ikiwemo kilimo cha mpunga kwa zaidi ya miaka minne sasa kwenye shamba namba 512 analomiliki kihalali kutokana na kikundi cha watu wakiwemo kutoka nje ya kijiji kuvamia maeneo hayo na kuanzisha mashamba pamoja na kujenga nyumba za kuishi.
Akizungumza kwa niaba ya mwekezaji huyo ambaye ni mke wa aliyewahi kuwa gavana wa benki kuu, Marehemu Daudi Balali,Bi Anna Muganda Balali,Msimamizi wa shamba hilo Mussa Christopher alisema wanamiliki shamba hilo la ekari 2000 kihalali, licha ya kesi mbalimbali zilizofunguliwa na baadhi ya wavamizi katika Mamlaka mbalimbali ambapo familia hiyo ilishinda.
Msemaji huyo wa familia ya Balali akaiomba Serikali kuweka mazingira Rafiki kwa wawekezaji wa ndani dhidi ya wawanaowakwamisha kwenye shughuli za uwekezaji kwasababu pindi wakiwezekeza licha ya kuwanufaisha wananchi wanaowazunguka kwa ajira na fursa zingine, watalipa Kodi na kukuza uchumi wa nchi.
Akabainisha licha ya vurugu zinazoendelea za mara kwa mara, mwaka Jana waliamua kutoa ekari 500 katika shamba hilo na kuamua Serikali ilipime na kuwapa wananchi kupitia Serikali ya kijiji, lakini kundi jingine la watu takribani 20 wakiwemo wavamizi kutoka nje ya kijiji walizuia zoezi hilo kwa kufanya vurugu.
Watu hao Agosti 6 mwaka Jana, walidaiwa kuchoma moto gari aina ya Landcruzer mali ya halmashauri ya wilaya ya Mlimba, pikipiki nne za viongozi wa vijiji walioambatana kwenda kwenye zoezi Hilo akiwemo Mwenyekiti wa kijiji Felician Lisakagu, Mwenyekiti wa kitongoji Evarist Lilonoka, Kaimu Mtendaji wa kijiji na Mwakilishi wa familia ya Balali walioongozana na watendaji wa halmashauri akiwemo Afisa mipango miji na vijiji wa halmashauri Remigi Lipiki, maafisa ardhi na mgambo watatu, kwenda katika zoezi hilo.
Watu hao pia walichoma.moto vifaa vya upimaji wa ardhi, simu na fedha zilizokuwa kwenye gari kwaajili ya kuwalipa posho watu waliokuwa waliifanya zoezi hilo pamoja na Mali zingine pamoja na kumjeruhi dereva wa gari hiyo ya halmashauri iliyochomwa Moto ambaye alitibiwa na baadaye kuruhusiwa.
Kikundi hicho licha ya kudaiwa kuvamia shamba hilo na kuendelea na shughuli za kilimo,na hata kuzuia wananchi kupitia Serikali ya kijiji wasipatiwe eneo na mwekezaji, kimedaiwa kuchochea vurugu, kunyang’anya bunduki ya Mlinzi wa shamba na kutoa taarifa za uongo za madai kwamba shmba hilo wanalimiliki kihalali bila kuwa na hati za umiliki.
Sakata hilo lilisababisha kufikishana mahakamani na kufunguliwa kwa kesi namba 3 ya mwaka 2022 katika mahakama ya hakimu mkazi kanda ya Morogoro mbele ya Jaji Kalunde dhidi ya mwekezaji huyo ambapo Mahakama alitupilia mbali shauri hilo na kutaka mwekezaji aendelee na uzalishaji baada ya kukosekana ushahidi usio na shaka.
“Baada ya kutupiliwa mbali kwa shtaka la awali, walifungua shauri jingine namba 10 la madai la mwaka 2022 mbele ya jaji Kwembe wakiwa watu 52 ambapo shauri hilo liliendelea mpaka tarehe 06 mwezi 10 ambapo mahakama ilisema mwekezaji hana kesi yeyote ya kujibu wala kushitakiwa, kualalamikiwa wala ya kudaiwa na kwamba mahakama haiwezi kumuhoji chochote na mtu yeyote nje ya mahakama haruhusiwi kumuhoji chochote”Alisema Mussa.
Hata hivyo akadai mawakili wa upande wa washtaki waliomba marekebisho ( amendment) ambapo wakati marekebisho yakiendelea mahamani mawakili hao wakaja na malalamiko kwamba wateja wao wananyanyaswa kwa kufanyiwa vitendo vya kikatili na jeshi la polisi ambapo mahakama iliwambia kuwa jeshi la polisi ni lazima liendelee na kazi yake kwani kuna mali za umma zimefanyiwa uharibifu.
Alisema vurugu hizo za mara kwa mara zimefanya mwekezajj kushindwa kuwekeza kwa wakati na kuikosesha Serikali mapato kutokana na kodi mbalimbali ambazo walitakiwa walipe katika kipindi chote cha uzalishaji.
Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Merela Bwana Dionis Ondole ambaye pia alishiriki katika zoezi la awali la.utoaji wa eneo hilo kwa aliyekuwa Gavana wa benki kuu Marehemu Balali alisema wavamizi hao ni wabishi kwani Serikali imekuwa ikiwafahamisha kwa muda mrefu kwamba eneo hilo ni la mwekezaji bila mafanikio.
“Viongozi wa Serikali wamekuwa wakisema kila wakati kuwa eneo hili ni la mwekezaji lakini hawa wananchi wachache wamekuwa wabishi mno na ndio hao wanaoanzisha vurugu na kusababisha watu wakosea amani.” alisema bwana Ondole.
Naye mjumbe wa Serikali ya kijiji hicho Simon Nicholaus alisema hali iliyopo kwa sasa ni mbaya kutokana na fujo kwenye shamba la mwekezaji Balali wakidai ni mali yao wakati mwekezaji Balali alikabidhiwa toka mwaka 2000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Fortunatus Musilimu licha ya kutotaka kuzungumzia malalamiko yaliyoripotiwa na chombo kimoja cha habari kuwa Polisi wananyanyasa wananchi kwa kuwakamata ovyo, alikiri kukamatwa na kushikiliwa kwa watuhumiwa watano wakiongozwa na Nkumbi Malashi Holela, wanaodaiwa kuhusika na uchomaji Moto gari ya halmashauri pikipiki, vifaa vya upimaji ardhi na Mali zingine wakati wa upimaji wa ardhi iliyotaka kumegwa wapewe wananchi.
Watu hao licha ya tuhuma zingine, pia wanatuhumiwa kupora silaha ya Mlinzi wa shamba la Balali, ambapo silaha hiyo baadaye ilikamatwa, pamoja na kutoroka dhamana katika kesi ya awali.