********************
Na Zillipa Joseph Katavi
Mama mjamzito anapaswa kula chakula bora kwa ajili ya kumwezesha mtoto aliye tumboni kuwa na afya njema.
Hayo yamesemwa na Afisa Lishe Manispaa ya Mpanda Thadeo Salum wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii juu ya mama mjamzito kutakiwa kula chakula chenye lishe toshelezi.
Thadeo alisema ulaji wa lishe bora ni ulaji wa vyakula unaozingatia makundi yote matano ya chakula, likiwamo kundi la nafaka kama mahindi, ulezi, ndizi mbichi, kundi la jamii ya mikunde na nyama kama maharage, kumbikumbi, kundi la mboga mboga kama mchicha, tembele, biringanya,n.k kundi la matunda kama maembe, machungwa n.k na kundi la asili ya sukari na mafuta kama miwa, asali karanga n.k.
Afisa lishe huyo pia alifafanua kuwa faida anazopata mama mjamzito kwa kula lishe bora ni pamoja kumuandaa mtoto atakayezaliwa kuwa na afya njema.
Aidha itamsaidia mama kuondokana na tatizo la kupungukiwa damu, pia kuongeza madini ya chuma, na kumwezesha mama kuwa na maziwa ya kutosha wakati amejifungua.
Aliongeza kuwa mama mjamzito mwenye kula chakula bora anapunguza uwezekano wa kuzaa mtoto mwenye udumavu, au mwenye uzito pungufu au kuzaa kabla ya wakati (premature birth).
Bi. Happiness Chesco ni mama mjamzito aliyepata nafasi ya kuzungumza na mwandishi wa habari hizi, amesema hii ni mimba yake ya pili na ameona tofauti kubwa tofauti na alipobeba mimba ya kwanza miaka saba iliyopita.
Ametaja tofauti hizo kuwa ni pamoja na kupata elimu ya kula vizuri vyakula vyenye afya kabla hajabeba ujauzito, hali anayosema imemsaidia sana kwani hata sasa hana hamu ya kula sana lakini kutokana na elimu aliyoipata kliniki anajilazimisha kula chakula chenye lishe toshelezi.
Sista Elida Machungwa ni Mratibu wa Afya ya mama na mtoto mkoani Katavi, alisema wakinamama wanapatiwa elimu ya lishe bora pindi wanapohudhuria kliniki kwa ajili ya vipimo na kujua maendeleo ya mtoto aliye tumboni.
Sista Machungwa pia amewaasa kinababa kujenga mazoea ya kwenda na wake zao kliniki ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayowasaidia katika malezi ya mtoto.