Picha mbalimbali za wawakilishi wa Taasisi ya Jamii Mpya Mkoani Pwani wakitoa msaada wa vitu mbalimbali katika hospital ya rufaa ya mkoa ya Tumbi.
……………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
TAASISI ya Jamii Mpya Mkoa wa Pwani, imetoa nguo za watoto na vitu mbalimbali kwa wagonjwa wenye mahitaji katika wodi ya wanawake na watoto ,Hospital ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi, ikiwa ni kufanikisha Kampeni ya FUNGA MWAKA KWA UPENDO.
Wakikabidhi msaada huo kwa uongozi wa hospital hiyo na wagonjwa ,Katibu wa Jamii Mpya Mkoani Pwani Rehema Kawambwa ameeleza, misaada hiyo ni sehemu ya mchango wao kwa kushirikiana na wadau.
“Moja kati ya malengo ya Taasisi ya Jamii Mpya ni kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi mbalimbali za Kitaifa na kuvitangaza ili kuhamasisha Watanzania kutembelea vya kwao na kupenda kufanya utalii wa ndani sanjali na kushiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii, sambamba na kuipa support” alielezea Rehema.
“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Uongozi mzima wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa kukubali ombi letu la kufika hospitalini hapa kuwajulia hali wagonjwa, na kuwapatia mahitaji”alieleza Rehema.
Vilevile Mratibu wa Taasisi hiyo Nicolas Mpandula amewashukuru viongozi wa Taasisi hiyo mkoa na wilaya, Daktari wa Meno Isaac Tarimo, Muuguzi Tumpefiki Minga, na Mkunga Mtaalamu Delila Msigwa kwa ushirikiano walioutoa.
Nae Mmoja kati ya wahitaji katika wodi hiyo Mama Latifa amesema yupo muda mrefu hospitalini hapo kutokana na watoto wake kusumbuliwa na tatizo la lishe duni.
Ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwathamini na kuwapa mahitaji ikiwemo sabuni za kufulia, sabuni za kuogea, pampers, dawa za meno, sukari, juisi, nguo za watoto .
Mama Latifa ameeleza,ana watoto mapacha wa kike wenye umri wa mwaka mmoja na miezi minne, wanasumbuliwa na Malnutrition (Lishe Duni),ambapo Taasisi hiyo imeomba jamii na wadau kuendelea kumsaidia mama huyo hadi hapo watoto wake watakapokuwa na afya njema ili aweze kuruhusiwa kutoka hospital.