Na. A/INSP FRANK LUKWARO
Mkoa wa Manyara umetajwa kushika nafasi ya pili kwa matukio mengi ya ukatili wa Kijinsia ambapo wakazi wa mkoa huo wametakiwa kutumia madawati ya Jinsia ili kuwafichua watu wanaofanya vitendo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere wakati wa uzinduzi wa Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto katika Kituo cha Polisi cha Orkesment Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ambacho kimejengwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya uzazi (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la Utu wa Mtoto (CDF).
Nyerere amesema mkoa huo unaongoza kwa mambo mazuri lakini kutajwa katika nafasi za juu kwa vitendo vya ukatili kunapaswa kukemewa ili kuondokana na nafasi hiyo ambapo amewataka Jeshi la Polisi kuzindisha mapambano katika kukomesha vitendo hivyo.
“Tumieni Dawati lililozinduliwa leo ili kukomesha vitendo hivi ambavyo vinatia aibu mkoa wet una hapa nawapongeza Jeshi la Polisi Pamoja na wafadhili waliofanikisha ujenzi wa jengo hili ambalo kwa kweli litaongeza chachu katika mapambano dhidi ya ukatili katika Wilaya ya Simanjiro” Alisema Makongoro
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jamii Faustine Shilogile alisema ofisi hiyo ya Simanjiro inafikisha jumla ya ofisi 58 ambazo zimejengwa katika nje ya vituo vya Polisi kutokana na mwongozo wa uanzishwaji wa madawati ya Jinsia na Watoto ambao unataka mazingira rafiki yanayozingatia usiri katika kutoa huduma kwa wahanga.
Alisema mkakati wa Jeshi la Polisi ni kuendelea kutoa huduma bora kwa kuweka mazingira bora ya utendaji kazi yanayomfanya mteja anapofika kutoa taarifa aweze kuwa na amani hivyo ujenzi wa madawati hayo utaendelea kwa kushirikiana na wadau wengine wanaopinga vitendo hivyo.
Naye Msaidizi wa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya uzazi (UNFPA) Dkt. Majaliwa Marwa amesema wamesaidia ujenzi wa ofisi hiyo ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia
Dkt. Marwa alisema Pamoja na madawati yaliyojengwa mkoa wa Manyara pia wamefanikiwa kusaidia ujenzi majengo ya dawati la Jinsia na Watoto nane katika mikoa ya Mara, Kigoma na Zanzibar ambapo hivi karibuni wanatarajia kukamilisha katika Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka amelipongeza Jeshi la Polisi Wilayani humo kwa hatua ambazo wamekuwa wakiendelea kuzichukua kwa watu wanaofanya vitendo vya ukatili ikiwemo vilivyotokea hivi karibuni katika Wilaya hiyo.
Pia amewaomba wazazi kutokubali kurubuniwa ili kuficha Ushahidi pindi Polisi wanapofanya kazi yao ya upelelezi jambo ambalo limekuwa likifanya kesi nyingi zinazoripotiwa kutokupata mafanikio chanya Mahakamani.