Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Miradi (TECU), Eng. Christian Mbise, wakati akikagua barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akipitia taarifa ya mradi wa barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), kwa kiwango cha lami, mkoani Kagera.
Kazi za ujenzi wa barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami zikiendelea, mkoani Kagera.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Kagera.
PICHA NA WUU
…………………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi,Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewatahadharisha Wakala wa Barabara Tanzania kupitia Kitengo cha Usimamizi wa miradi cha Tanroads Consulting Engineering Unit (TECU), kuwa Serikali haitegemei miradi ya barabara inayosimamiwa na Kitengo hicho kufeli kabla ya wakati wake.
Amezungumza hayo mkoani Kagera, wakati akikagua barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami na kutekelezwa na mkandarasi kutoka kampuni ya China Road and Bridge Cooperation kwa muda wa miezi 30.
“Kwenye mkataba kuna vipendele vingi vimetajwa hivyo hatutegemei barabara hii ijengwe halafu iharibike kabla ya muda na ndio maana tupo hapa kuwakumbusha kila kitu kifanyike kama mkataba unavyosema na kwa muda uliopangwa”, amesisitiza Eng. Kasekenya.
Naibu Waziri huyo pia amemuagiza mkandarasi huyo kuongeza vifaa vya ujenzi pamoja na wataalam ili kuharakisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba, 2024.
“Barabara hii kimsingi ni kama ya Afrika Mashariki kwani inakwenda kufungua mkoa wa Kagera, kuunganisha nchi ya Tanzania, Uganda, Burundi na Sudani Kusini hivyo inategemea kubeba mizigo mikubwa na matarajio ya Serikali ikamilike kwa wakati na viwango vya ubora”, amefafanua Kasekenya.
Aidha, amesema malipo yote ya awali kwa mkandarasi kiasi cha shilingi Bilioni 13 yamekwishalipwa kwa wakati na hivyo Serikali haimtegemei yeye kuwa na sababu zozote za kukwama kuanza ujenzi.
Kasekenya, ametoa wito kwa mkandarasi kutoa fursa za ajira kwa wananchi waliopo maeneo hayo ili kuinua uchumi wa wananchi wanaopitiwa na mradi huo.
Amesisitiza kwa kitengo cha TECU kuhakikisha mkandarasi anatekeleza jukumu la kusaidia masuala ya kijamii katika maeneo ya mradi (Social Responsibilities) ikiwemo ujenzi wa hospitali, mabweni, kuchimba visima, na shule ili jamii nayo ionje matunda ya miradi hii ambayo Serikali inatoa fedha nyingi.
Awali akitoa taarifa ya mradi Mhandisi Mshauri kutoka TECU, Eng. Christian Mbise, ameeleza kuwa mradi huo umeanza mwezi Mei mwaka huu na mpaka sasa ujenzi wa kambi ya mkandarasi umekamilika kwa asilimia 100 na bado mkandarasi anaendelea na ujenzi wa wa kambi ya mhandisi mshauri, kuleta mitambo na mashine pamoja na kuongeza wataalam.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Bugene – Burigi Chato Sehemu ya Hifadhi ya Taifa (km 60), unatarajia kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 109 pamoja na VAT.