Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, (mwenye joho jekundu), akitunuku Astashahada Stashahada na Shahada ya kwanza kwa wahitimu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini katika mahafali ya 36 duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Martha Qorro na Kulia kwake ni Mkuu wa chuo hicho Prof. Hozen Mayaya na
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, akimtunuku cheti mwanafunzi bora Ali Shafii Shaban aliyeongoza kwa kupata matokeo ya GPA ya 5, katika mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, akiweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa jengo la maktaba la Chuo katika mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Martha Qorro, akifuatiwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo Kanza ya Ziwa Mwanza Prof. Juvenal Nkonoki.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, (mwenye joho jekundu) akiwa katika akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini baada ya kuhitimisha hafla ya mahafali ya 36 duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Mwanza)
********************
Na. Ramadhani Kissimba na Saidina Msangi, WFM, Mwanza
Serikali imewataka wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kuchangamkia fursa ya upendeleo inayotolewa na sheria ya manunuzi inayozitaka taasisi zote za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za manunuzi ya mwaka kwa ajili ya makundi maalum katika jamii wakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Rai hiyo imetolewa jijini Mwanza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo ambaye alimwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika mahafali ya 36 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza.
Bi. Omolo alieleza kuwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Bajeti kuu ya Serikali hutumika kwenye manunuzi mbalimbali ya bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi na hivyo ni vema wakachangamkia fursa hiyo.
‘‘Bajeti ya manunuzi kwa mwaka huu wa fedha ni takribani Sh. trilioni 32, ambapo asilimia 30 ya kiasi hiki ni takribani sh. trilioni 9.78 ambazo zinapaswa kutengewa makundi haya maalum. Hivyo, niwaase vijana wetu kujiunga katika makundi na kuyasajili rasmi ili yatambulike kuweza kunufaika na fursa hiyo’’, alisema Bi. Omolo.
Alifafanua kuwa Serikali iko tayari kusaidia vijana wenye mawazo chanya ya kibiashara kutimiza malengo yao jambo la msingi ni kujiunga kwenye vikundi vyenye lengo la aina moja ili iwe rahisi kukabiliana na changamoto ya mtaji mdogo kwa kushirikiana na wenzako katika kikundi kuliko mtu akiwa peke yake.
Bi. Omolo aliwaasa wahitimu kuwa na moyo wa uthubutu na kuyafanyia upembuzi yakinifu mawazo yao ya biashara, kuyaandalia mpango wa biashara na kuyatekeleza kwa ufanisi bila kukata tamaa kwani ulimwengu wa leo unahitaji moyo wa kupenda kuendelea kujifunza na zaidi kuwa wabunifu.
Alitoa rai kwa wazazi na walezi kuiunga mkono Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wahitimu hao kwa kuwawezesha watakaokuwa na mawazo ya kibiashara kupata mitaji ya kuanzisha miradi yao ya biashara.
‘‘Serikali kwa upande wake itaendelea na agenda yake ya kuboresha mazingira ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya vijana kupitia mikopo inayotolewa na mamlaka za serikali za mitaa’’ alisema Bi. Omolo.
Pia Bi. Omolo alizitaka Bodi za taasisi zote za umma kuzisimamia vizuri taasisi zinazotekeleza miradi ya ujenzi ili thamani ya fedha ionekane kwani palipo na usimamizi mzuri wa miradi ya ujenzi Serikali haitasita kutoa fedha za maendeleo.
Aidha, alitoa rai kwa taasisi nyingine za elimu ya juu na kati na ikiwezekana shule za sekondari kuiga mfano wa chuo hicho wa kuwaandaa wataalamu kuwa mahiri na weledi kwa kutumia mfumo unaohusisha nadharia na vitendo, vilevile kozi zenye moduli ya masuala ya ujasiriamali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Martha Qorro, ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo kuwezesha chuo hicho kutekeleza kwa ufanisi mradi wa upanuzi wa chuo.
Pia alisisitiza kuwa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho litaendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kukisimamia chuo hicho kuboresha mazingira yake na miundombinu huku likitanguliza maslahi mapana ya Taifa ili kukiwezesha chuo kupata mafanikio zaidi.
Naye Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo ya Vijijini Prof. Hozen Mayaya, alisema kuwa wahitimu hao wamefundishwa na wamefuzu kuweza kuingia katika kutumikia Taifa wakiwa na maarifa na ujuzi stahiki katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa chuo hicho kimejidhatiti katika kuwaandaa wataalamu wenye weledi wa kutosha katika fani za mipango ya maendeleo, bali pia kutoa huduma iliyo bora kwa wakati na inayokidhi matakwa ya wadau.
Aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendelea kukiwezesha Chuo kupata miundombinu ya msingi ambayo ni bora na ya kisasa ikiwemo majengo yaliyowekewa mawe ya msingi na uzinduzi.
Jumla ya wahitimu 2691 wakiwemo wanawake 1491 na wanaume 1200 wamehitimu mafunzo yao na kutunukiwa Astashahada Stashahada na Shahada ya kwanza kwa wahitimu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini katika programu 3 kwenye mahafali ya 36 ya Chuo duru ya pili katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza.