Ziara ikiendelea.
Aliyevaa miwani na kofia kulia ni Kamshna Msaidizi Uhifadhi,Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo akiteta jambo na Mwandishi wa Global TV Ibrahim Kunoga wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea hifadhi ya Taifa ya Saadani.Mwandishi wa Habari Mashaka Kibaya akiwa ndani ya bodi maalumu wakati wa ziara hiyo.
Majadiliano yakifanyika katika ziara hiyo.
Waandishiwa habari wakiwa ndani ya boti wakati wa ziara hiyo.
Na Mashaka Kibaya, Tanga.
HIFADHI ya Taifa ya Saadani ni Mbuga pekee ambayo mazingira yake yameungana
na Bahari ikiwa na Ikolojia ya mbuga na ile ya bahari huku ikiwa imesheheni
wanyama wa aina mbalimbali.
Miongoni mwa Wanyamapori wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni Chui, Nyati,
Tembo, Pundamilia, Kuro na wengine wengi hivyo si jambo la ajabu kumkuta Simba
akiwa anapunga upepo kwenye fukwe za Bahari ya Hindi.
Kivutio kingine kinachoipatia umaarufu mkubwa hifadhi hiyo ni uwepo wa
fungu la mchanga ‘Mafui’. Aina ya tabaka la ardhi linalopatikana katikati ya
maji eneo ambalo ni kina kirefu, sehemu ambayo mazingira yake huvutia wageni
kutembelea.
Mambo yanayopatikana ndani ya Mafui, ni viumbe hai kama vile Kasa, mawe
aina ya Matumbawe yenye rangi na maumbo tofauti ambayo ni mazalia ya Samaki
eneo ambalo kisheria ni sehemu rasmi ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Pia kuna mazingira rafiki yenye umbo la bakuli linalowawezesha watalii
kuogelea na hata wale wasioweza wanaweza kutumia eneo hilo kujifunza mchezo huo
wa kuogelea ambao umetokea kupendwa sana ulimwenguni.
Kwa wageni au watalii hawawezi kulifikia
eneo hilo la Mafui ambalo linafahamika kwa jina maarufu la ‘Mwali’
ambapo waatalazimika kutumia usafiri wa boti ili kwenda kujionea mambo mazuri
yenye kupendeza.
Kwa nini Mafui imebeba umaarufu wa jina Mwali? Ni kwa sababu kuna wakati
imekuwa ni vigumu sana kuliona tabaka hilo la ardhi lililopo kwenye kina kirefu
cha Maji, hadi pale utakapofanikiwa kufuata ratiba maalum ambayo huzingatiwa na
watembeza wageni ‘Tour Guide.
Kwa vile Mafui inahitaji kufuata ratiba maalum pasipo kuivuruga ndipo
kuiona, wale wasiozingatia kanuni zake hushindwa kuliona eneo hilo, hivyo
kiasilia ama tamaduni ikafananishwa kana kwamba unataka kumuona bibi Harusi
ambapo kuna taratibu maalum ili kuruhusiwa kumuona.
” Kuna wakati kumuona ‘Mwali’ (Mafui) ni changamoto, utaiona Mafui
hadi pale maji yanapokupwa, hivyo wageni wanaotembelea wakifanikiwa kuliona
tabaka hilo la ardhi hufurahi sana” anasema Ephraim Mwamongo Kamishna
Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Anaongeza kusema Mwali anapoonekana wageni hujawa na furaha ambapo wanaweza
kulitumia eneo hilo kwa kuvishana pete za uchumba, harusi na hata kupumzika tu,
watu wakipiga picha na kufurahi mandhari mbalimbali yaliyopo.
Katika kumuongezea thamani Mwali (Mafui), Mwamongo alisema, upo mpango wa
kujenga Dock Yard ili vyombo vya Usafiri kama boti kuegesha na kuwawezesha
wageni kupanda na kusafiri kuweza kwenda kuona Mwali.
Mwamongo anatanabaisha kuwa, Hifadhi
ya Taifa ya Saadani imefanikiwa kiwa na
vijana mahiri waliobobea katika kuwaongoza na kuhudumia wageni wakiwawezesha
kufurahia ziara zao wakihisi hawajapoteza kitu.
Kimsingi Hifadhi ya Taifa ya Saadani inaelezwa kuwa salama na shirikishi kwa wananchi wanaoishi vijiji
jirani ambao wamekuwa wakinufaika kwa kupatiwa
miradi mbalimbali ya maendeleo.
Manufaa mengine wanayopata wananchi wa eneo hilo kupitia uwepo wa hifadhi
ya Saadani kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, ambapo
askari waliopo kwenye hifadhi wamekuwa wakihusika kuhakikisha usalama wa jamii.
Vile vile hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani imekuwa fursa adhimu ambapo
wenyeji hususani wavuvi wamekuwa wakiitumia kama Soko kuu kwa ajili ya kuuzia
Samaki wao kwa kuwa wageni wanaotembelea eneo hilo hushawishika kununua bidhaa
hizo kwa wenyeji wao.
Ili kuiwezesha hifadhi yaTaifa ya Saadani kuendesha shughuli zake kwa tija,
kazi ya uboreshaji wa miundombinu imeendelea kufanyika na kwa njia ya reli,
barabara, ndege na hata maji zimefanyiwa kazi hatua ambayo imelenga kurahisisha
usafiri kwa wageni kutoka sehemu tofauti.
Kamishna Msaidizi uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo
anasema, kupitia kituo ‘Station’ ya reli Mvave wageni wanaweza kufika kwenye
eneo la hifadhi hiyo inayoondokea kuwa
na umaarufu mkubwa duniani.
Mwamongo anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan
kuwawezesha kupata fedha zilizosaidi kufanya maboresho ya miundombinu.
Ni kupitia fedha za COVID hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani imeweza
kunufaika ambapo kwa upande mwingine Mwamongo amemshukuru na kumpongeza Rais
Samia kwa hatua yake kufanya Filamu ya Royal Tour.
Kamishna Msaidizi Mwamongo anasema kwamba, Royal Tour ya Mama Samia Suluhu
Hassan imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii kwenye
hifadhi ya Taifa ya Saadani ambapo anatoa wito kwa watanzania kujenga utamaduni
wa kutembelea hifadhi hiyo ya kipekee.