****************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga na kujiimarisha vizuri kuelekea mwisho wa mwaka 2022 katika suala zima la ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Ameyasema hayo kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Benjamin Kuzaga wakati wa ukaguzi rasmi wa makao makuu ya Polisi uliofanywa na Naibu Kamishna wa Polisi kutoka kitengo cha ufuatiliaji na tathimini DCP GABRIEL SEMIONO aliyeongozana na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia nchini ACP PAUL SANGA.
Kamanda Kuzaga amewahakikishia ulinzi na usalama wakazi wa mkoa wa Mbeya na kusema kuwa “Jeshi la Polisi linafanya mazoezi ya utayari na mazoezi ya kivita ikiwa ni sehemu ya kujiweka tayari kiusalama”
Aidha Kamanda Kuzaga amewatoa wasiwasi wananchi na wakazi wa mkoa wa Mbeya kufuatia mazoezi hayo na kusema kuwa ni sehemu ya kujiweka vizuri. Pia ametoa rai kwa wakurugenzi kutoa maeneo maalum kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi.
MADEREVA BAJAJI JIJI LA MBEYA WATAKIWA KUJALI USALAMA WAO NA WATUMIAJI WENGINE WA BARABARA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewataka madereva wa bajaji jiji la Mbeya kujali usalama wao na usalama wa watumiaji wengine wa barabara kwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Akizungumza Disemba 14, 2022 katika kikao kilichohusisha wamiliki na madereva bajaji jiji la Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga amesema lengo la kikao hicho ni kukumbushana sheria za usalama barabarani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.
Aidha kamanda Kuzaga amewaomba madereva na wamiliki wa bajaji wa Jiji la Mbeya kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi hususani katika suala la utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Kwa upande wao wamiliki wa bajaji wamelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa maelekezo, miongozo na elimu iliyotolewa kuhusu suala la usalama barabarani kwa madereva bajaji.