Muonekano wa jengo la Mheshimiwa Jaji Kanda ya Shinyanga linalojengwa na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 mkoani humo.
Muonekano wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu linalojengwa na Vikosi vya Ujenzi na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 65 mkoani Shinyanga.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Shinyanga Eng. Nestory Nanguka (kushoto), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (kulia), wakati akikagua ujenzi wa jengo la Mheshimiwa Jaji Kanda ya Shinyanga linalojengwa na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85, mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (kushoto), akitizama ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu linalojengwa na Vikosi vya Ujenzi na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 65 mkoani Shinyanga. Kulia ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Shinyanga Eng. Nestory Nanguka.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Shinyanga Eng. Ferdinand Mdoe, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akikagua Daraja la Negezi (m 60), katika barabara ya Kanawa – Mihama lililojengwa na kukamilika kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.8, mkoani humo.
Muonekano wa Daraja jipya la Negezi (m 60), katika barabara ya Kanawa – Mihama lililojengwa na kukamilika kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.8, mkoani Shinyanga. Kushoto kwake ni Daraja la Awali la Negezi la njia moja.
PICHA NA WUU
………………………………
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ametoa mwezi mmoja kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa jengo la Mheshimiwa Jaji Kanda ya Shinyanga ili aweze kuhamia na kutumia jengo hilo.
Amezungumza hayo mkoani Shinyanga mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo pamoja na jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu linalojengwa na Vikosi vya Ujenzi na kusimamiwa na Wakala huo ambapo amesisitiza Wakala huo kujenga majengo bora yatakayodumu kwa kipindi kirefu.
“Hakikisheni mnamsimamia mkandarasi ili ajenge kwa viwango hivyo hivyo vilivyopo katika usanifu”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Awali akitoa taarifa ya miradi hiyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Shinyanga Eng. Nestory Nanguka, ameeleza kuwa mpaka sasa utekelezaji wa jengo la Mheshimiwa Jaji Kanda ya Shinyanga umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kishapu umefikia asilimia 65.
Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi ambapo atakagua miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amekagua Daraja la Negezi (m 60) katika barabara ya Kanawa – Mihama lililojengwa na kukamilika mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.8.
Amesema Serikali iliamua kujenga daraja hilo kubwa kutokana na uwepo wa daraja dogo lililojengwa toka mwaka 1954 ya njia moja ambalo halikukidhi mahitaji ya wananchi na kusababisha adha kubwa hasa kipindi cha masika.
Kasekenya amewataka wananchi hao kulitunza Daraja hilo kwa kutofanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa daraja.
Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi ambapo atakagua miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.