Na Mwandishi wetu, Mirerani
WADAU wa madini nchini hususani wachimbaji wa Tanzanite wametakiwa kuchangia shughuli za kijamii kwani ni takwa la kisheria na siyo hisani.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameyasema hayo akifungua warsha ya madiwani, asasi za kiraia, viongozi wa Halmashauri na wachimbaji madini ya matumizi ya takwimu zinazotolewa na taasisi ya uhamasishaji, uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia (TEITI) mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
Mbibo amesema wadau wa madini kusaidia jamii (CSR) ni takwa la kisheria hivyo makampuni na wachimbaji kwa ujumla wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuwajibika kwa jamii.
“Mnapofanya shughuli za uchimbaji madini sehemu husika mnakuwa mmepishwa na wakulima au wafugaji waliokuwa wanafanya shughuli zao hapo, hivyo mnapaswa kusaidia jamii inayowazunguka,” amesema Mbibo.
Amesema wadau hao wanapaswa kusaidia jamii inayowazunguka kupitia miundombinu ya barabara, elimu, afya au maji ili wanufaike kupitia shughuli wanazozifanya.
Kaimu katibu mtendaji wa TEIT, Mariam Mgaya amesema kupitia warsha hiyo wadau wa madini watajengewa uelewa na uwezo zaidi juu ya upatikanaji wa taarifa za madini, mafuta na gesi asilia.
Ofisa Tarafa ya Moipo, Joseph Mtataiko amesema wadau wa madini ya Tanzanite wengi wao wana mwamko mdogo wa kusaidia jamii inayowazunguka kupitia CSR.
“Mchimbaji maarufu wa madini Bilionea Saniniu Laizer ndiye amewatoa kimasomaso wachimbaji wa Tanzanite kwa kujenga shule na kukabidhi kwa serikali na siyo kwa sababu amepata fedha nyungi ni wito wake tuu,” amesema Mtataiko.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani Rachel Njau amesema elimu inapaswa kutolewa kwa wadau ili waweze kutimiza hilo kwani wengjne wanatoa kimya kimya bila kujulikana.
Mchimbaji wa madini Hosea Pallangyo amesema pamoja na kutaka wachimbaji kuchangia jamii pindi wakipata madini pia waangaliwe gharama walizochimba kwani wengine wametumia miaka 10 kuchimba bila kupata.