NJOMBE
Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Itracom kutoka Nchini Burundi inatarajia kuzindua kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha mbolea tani milioni moja hapo Disemba 16 mwaka huu, hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa mbolea na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Kiwanda hicho kilichojengwa Dodoma kimetajwa kuzalisha mbolea za FOMI za aina tatu ikiwemo ya kupandia ,kukuzia na kunenepesha pamoja na chokaa ambayo itaenda kuwa tiba kwenye udongo ambao umeharibiwa na tindi kali.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa mawakala wa pembejeo za kilimo kutoka mkoa wa Njombe ambayo imefanyika mjini Makambako Mkurugenzi wa biashara na maendeleo ya masoko wa kiwanda cha mbolea cha itracom Dokta Kenneth Masuki amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka
Meneja wa utafiti na ubunifu wa kiwanda hicho Elias Nyongabo amesema mbolea hizo zina ubora unaotakiwa kwa kuwa zimefanyiwa utafiti kwenye mazao ya Mahindi ,maharage,mpunga, alizeti ,mtama,mihogo na viazi na zimekua na tija kubwa.
Kwa upande wake Meneja biashara na Masoko kutoka kampuni ya Bens Agrostar Co.Ltd ambayo imepewa kazi ya kusambaza mbolea za Itracom Dokta JULIUS NAMBUA amesema atahakikisha mbolea hizo zinawafikia wakulima kwa wakati ili waongeze kasi ya uzalishaji kwenye mazao yao.
Nao baadhi ya mawakala wa pembejeo za kilimo mkoani Njombe akiwemo Roza Makweta na Ambele Mwaipaja wamesema kiwanda hicho kimekuja wakati mwafaka na kitaenda kuondoa utegemezi wa kutegemea mbolea kutoka nje ya nchi
Kujengwa kwa kiwanda hicho mkoani Dodoma kunakwenda kuwa muarobaini wa upatikanaji wa Mbolea hapa nchini na kuwakomboa wakulima ambao wamekuwa kwenye changamoto kubwa tangu kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Corana mwaka 2019 hadi vilipotokea vita vya Ukraine na Urusi.