************************
Na Anjela Seth.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani ( FCC) Dkt William Erio ametoa wito kwa Wazalishaji wa bidhaa hapa nchini kuhakikisha bidhaa zao wanaziweka kwenye mwonekano mzuri ili kuwavutia wateja pamoja na kukabiliana na ushindani wa soko.
Dkt Erio ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kilele cha maonyesho ya Viwanda vya Ndani yanayofanyika kwenye viwanja Sabasaba jijini Dar es salaam ambapo amesema changamoto kubwa iliyopo kwasasa kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ni mwonekano usio vutia.
“FCC tunawaomba wazalishaji wa bidhaa pamoja nakwamba wanazingatia ubora wa bidhaa lakini kitu kingine cha msingi wazingatie muonekano(Design) mzuri kwenye bidhaa zao kwani inasaidia sana kumvutia mteja aweze kununua bidhaa hiyo nakuweza kutangaza bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi” amesema Dkt Erio.
Aidha amesema kuwa Tume ya Ushindani( FCC) imekua ikitoa elimu kwa wafanyabiashara na Wazalishaji wa bidhaa kuzingatia ubora lakini changamoto ambayo imeonekana kwa sasa ni hali ya kuwepo kwa bidhaa ambazo hazina mwonekano mzuri (Designe) hali ambayo inachangia kushindwa kuwavutia wateja kwenye soko.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa FCC pia amewashauri Watanzania ambao wanandoto za kuwekeza viwanda lakini hawana mitaji au teknolojia wajinga na wawekezaji wengine kutoka nje ya nchi ili kuwafanya wapate mtaji au teknolojia nakuweza kwa kiwango wanachotaka.
Kuhusu utoaji wa Elimu ya Biashara kwa Makundi Maalumu Dkt Erio amebainisha kwamba tayari FCC imekutana na Viongozi wa Chama Cha Watu wenye Ulemevu wa kutokusikia (VIZIWI) nakuwapatia mafunzo ya namna ya kuzingatia uzalishaji wa bidhaa bora na jinsi ya yakuepukana na matumizi ya bidhaa bandia, nakwamba hivi karibuni Tume hiyo inatarajia kukutana na Watu wenye Ulemavu wa macho(VIPOFU) ili wawapatie elimu hiyo.
Tume ya Ushindani (FCC) ni chombo cha Serikali kinachojitegemea kilichoundwa kwa sheria ya Ushindani namba 8 ya Mwaka 2003 (FCA) ili kuhamasisha na kulinda ushindani katika shughuli za kibiashara na kumlinda mtumiaji wa bidhaa na huduma dhidi ya mwenendo usio wa haki na wa upotoshaji katika soko.