Tenki la maji linaloendelea kujengwa ambalo linatarajiwa kuhudumia wananchi wa vijiji viwili vya Ifuwa na Wotalisoli wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Kilolo Obed Ngonde akizungumza na baadhi ya wananchi na viongozi wa kijiji cha Ifuwa na Wotalisoli kwenye eneo la ujenzi wa mradi wa maji unaoatarajiwa kuhudumia wananchi wa vijiji hivyo.
…………………….
Na Muhidin Amri,Kilolo
WIZARA ya maji kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),imetenga Sh.bilioni 1,908,564,878.00 kwa ajili ya kujenga mradi wa maji utakaowanufaisha zaidi ya wakazi 3,541 wa vijiji vya Ifuwa na Wotalisoli Halmashauri ya wilaya Kilolo mkoani Iringa.
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Kilolo Obed Ngonde alisema,fedha hizo zitumika kutekeleza mradi huo ambao utamaliza kero ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu kwa wakazi wa vijiji hivyo ambao hawajawahi kupata maji ya bomba tangu vijiji hivyo vilipoanzishwa.
Ngonde alisema,lengo la mradi huo ni kuwapatia wananchi wa vijiji vya Ifuwa na Wotalisoli maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 pamoja na kupunguza mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayoweza kujitokeza kutokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama.
Kwa mujibu wa Ngonde,muda wa ujenzi wa mradi huo ni miezi sita na ulianza kujengwa tangu mwezi Juni 2022 na unatarajiwa kukamilika tarehe 20 Machi 2023 na muda wa matazamio utakuwa siku 365.
Alisema, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 45 na mkandarasi ameshalipwa Sh.milioni 286,284,731.70 kati ya Sh.bilioni 1.9 ikiwa ni malipo ya awali.
Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Ruwasa wilaya ya Kilolo ilipokea kiasi cha Sh.bilioni 1,624,000,000 kwa ajili ya kujenga miradi ya maji katika vijiji sita vya Ruhaha Mbuyuni,Image,Mtandika,Mgowole na Mahambala.
Alisema, katika bajeti ya 2021/2022 kazi zote zimetekelezwa kwa kutumia wataalam wa Ruwasa kwa kushirikiana na mfundi wadogo ambao kwa sehemu kubwa walitoka ndani ya mkoa wa Iringa.
Pia alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wamepanga kutekeleza miradi mitatu katika kijiji cha Kimala,Ifuwa-Wotalisoli na upanuzi wa mradi wa maji kijiji cha Wamingeto na fedha zilizotengewa kwa ajili ya miradi hiyo ni Sh.bilioni 4,666,569,712.76.
Ngonde alieleza kuwa,katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini sheria inataka mwananchi apate huduma ya maji umbali usiozidi mita 400,hata hivyo Ruwasa inasisitiza ni vyema wananchi wakavuta maji majumbani badala ya kutumia vituo vya kuchotea maji kama ilivyo lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ifuwa,wameiomba Serikali kumsimamia kwa karibu mkandarasi Kampuni ya Koberg Contruction Co Ltd inayejenga mradi huo ili akamilishe kazi hiyo haraka na wananchi wapate huduma ya maji katika maeneo yao.
Zamda Kalinga mkazi wa kijiji cha Ifuwa alisema,changamoto ya maji ni ya muda mrefu na bado wanaendelea kuteseka na kutumia muda mrefu kwenda kutafuta maji yanayopatikana kwenye mito na vyanzo vingine vya asili.
Amemuomba mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike haraka na ikiwezekana hata kabla ya muda wa mkataba ili wananchi waanze kupata maji safi na salama.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ifuwa Daud Hugi,ameishukuru serikali kuleta mradi huo ambao utamaliza kero ya maji na usumbufu kwa wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya kazi nyingine za maendeleo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Wotalisoli Boniface Mkimbo alisema,kijiji cha Wotalisoli na Ifuwa tangu kuumbwa kwa Mbingu na Ardhi havijawahi kupata maji ya bomba,hivyo kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni faraja kubwa kwao.
Alisema,kwa sasa wananchi wa Wotalisoli wanalazimika kutembea kati ya km 1.5 hadi 2 kwenda kutafuta maji kwenye mito na visima vya asili ambavyo wakati mwingine vinakauka kutokana na ukame uliopo hasa majira ya kiangazi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa mkandarasi wa kampuni ya Koberg Contruction Co Ltd Mhandisi Choma Magesa alisema,katika utekelezaji wa mradi huo changamoto kubwa ilikuwa kufika kwenye chanzo ili kupata njia ya kulaza mabomba hadi kwenye tenki.
Hata hivyo alisema,changamoto hiyo imemalizika baada ya kupata nguvu ya wananchi ambao walishiriki kuchimba mtaro wa kulaza mabomba na matarajio yao hadi kufikia mwezi Januari 2023,wananchi wataanza kupata huduma ya maji kwani mradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.