WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) jijini Dodoma leo wakati akitoa matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2022. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni.
………………..
Na. Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora, Jenista Mhagama amesma kuwa kiwango cha uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma kwa mwaka huu kimeongezeka hadi kufikia asilimia 75.9 ikilinganishwa na uliofanyika mwaka 2014 ambao kiwango kilikuwa asilimia 66.1.
Hayo ameyasema leo Desemba 9,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari akitangaza matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma kwa mwaka 2022.
Waziri Mhagama amesema kuongeza kwa matokeo hayo yanatokana na jitihada za kuimarisha uzingatiaji wa maadili chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
”Matokeo ya utafiti huu yanaonesha juhudi za serikali za kuchukua hatua mbalimbali za kuweka misingi imara ya usimamizi wa maadili, kuweka mazingira wezeshi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.’amesema Waziri Mhagama
Aidha amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, kufanya kikao kazi cha pamoja na wadau kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kina kuhusu matokeo ya utafiti huu na kuja na mikakati ya ufuatiliaji wa uzingatiaji wa maadili katika sekta zote kulingana na matokeo.
Pia amewataka Waajiri wahakikishe wanatenga bajeti ya mafunzo ya maadili na kuendesha mafunzo kwa watumishi wa umma walio kazini na wale wanaoajiriwa.
Waziri Mhagama Amesisitiza kuwa kuajiri wanaweka na kuimarisha mifumo ya utoaji wa mrejesho ndani ya taasisi zao ili kuendelea kutoa fursa kwa wananchi kukemea vitendo vya ukiukwaji wa Maadili.