NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU kutoka katika sekta mbalimbali wametakiwa kujitokeza na kudhamini kazi za kibunifu za Kisayansi zinazofanywa na wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari Tanzania bara na visiwani.
Ameyasema hayo leo Desemba 8,2022 Jijini Dares Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi, Prof.Evaristo Liwa, alipomwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Aldof Mkenda katika hafla ya kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika maonyesho ya kazi za kibunifu za kisayansi yanayoratibiwa na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi(YST) katika shule za sekondari Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Prof.Liwa amesema “Nimefurahishwa kuona vijana wadogo wakibuni miradi mikubwa na mizuri kama hii kupitia sayansi wanayoipata shuleni, kwa kweli wamenishangaza na hili ni jambo kubwa ambalo tukiliendeleza litatupatia wanasayansi wengi na wazuri wa kutatua matatizo katika nchi yetu”.
Pamoja na hayo amesema itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kuhakikisha kazi za kisayansi zinazobuniwa na wanasayansi chipukizi zinaendelezwa ili ziweze kusaidia jamii na taifa kwa ujumla hapo baadae.
“Ninaamini kwamba kama Waziri wa Elimu angekuwapo hapa leo, angetoa tamko kubwa, asingevumilia kuwaacha hawa vijana hivi hivi kwa kazi hizi nzuri walizofanya, ila itoshe tu kusema kwamba hii ni hazina kubwa na Waziri ameniagiza niwaambie kwamba wizara yake itaendelea kutengeneza mazingira mazuri yakuendeleza kazi zenu hizi za kibunifu mnazofanya ili zitumike katika kutatua matatizo kwenye jamii.” Amesema
Nae Mwanzilishi mwenza wa YST, Dkt.Gozibert Kamugisha, amesema kwa miaka 12 mfululizo wamekuwa wakiibua vipaji vya wanafunzi kutoka katika mikoa mbalimbali kwa kuwawezesha kubuni miradi mbalimbali ya kisayansi inayolenga kutatua matatizo kwenye jamii inayowazunguka.
Amesema tayari kazi hizo zimeanza kuleta matokeo chanya kwa kuwavutia wanafunzi wengi kupenda masomo ya sayansi na kwamba wanaofanya vizuri zaidi wamekuwa wakipata zawadi za udhamini wa masomo ya vyuo vikuu, kupewa medali, pesa tasilimu na wengine kupelekwa nje ya nchi kwenda kushiriki na kushindania tuzo za miradi ya kisayansi.
“Na kote huko wamekuwa wakifanya vizuri.Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza wanasayansi wengi nchini na tunataka kila mwanafunzi kabla ya kumaliza kidato cha nne awe amebuni kitu chochote chenye tija katika jamii, hiyo ndiyo sayansi tunayoitaka,”Amesema Dkt.Kamugisha.
Nae Ofisa Mtendaji wa Shirika la Karimjee Jivanjee Foundation ambao ni wadhamini wakuu wa maonyesho hayo, Bi.Caren Rowland, amesema mpaka mwaka jana shirika hilo limedhamini wanafunzi 37 kwenda vyuo vikuu na mwaka huu watadhamini wengine wanne wanaoshinda katika maonyesho hayo ya YST kwenda kusoma katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu masuala ya sayansi na kwamba lengo ni kujenga msingi kwa wanafunzi hao kuwa na ari ya kitaaluma na kupenda masomo ya sayansi.