Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (mweye fulana nyeupe) akiwa na baadhi ya watumishi wa Taasisi hiyo wakishiriki zoezi la usafi katika fukwe ya Msasani Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya sherehe za kumbukizi ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika pamoja na siku ya kutoa kwa jamii (Giving Tuesday).
Wananchi wa Msasani Bonde la mpunga pamoja na wakishirikiana na Baadhi ya watumishi wa FCS pamoja na wadau wengine wa Mazingira kufanya usafi ikiwa ni sehemu ya sherehe za kumbukizi ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika pamoja na siku ya kutoa kwa jamii (Giving Tuesday).
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga akipanda mti katika fukwe ya msasani Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bonde la Mpunga Msasani Hemedi Chamwana akishiriki zoezi la kupanda mti kwaajili ya utunzaji wa mazingira katika fukwe ya Msasani leo Disemba 9,2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha zoezi la kufanya usafi na upandaji miti katika fukwe ya Msasani Jijini Dar es Saalam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na Mazingira ya ECCT Lucky Michael akizungumzia ushiriki wao katika zoezi hilo lililokwenda sambamba na ugawaji vyeti kwa wanafunzi 25 waliohitimu mafunzo ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira.
Na: Hughes Dugilo, DSM
Shirika la asasi za kiraia nchini (FCS) kwa kushirikiana na asasi ya nipe fagio, na ECCT wameshiriki zoezi la kufanya usafi sanjari na kupanda miti katika fukwe za Msasani jijini Dar es Salaam ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni juhudi za kuunga mkono sherehe za kumbukizi ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika pamoja na siku ya kutoa kwa jamii (Giving Tuesday) ambayo hufanyika kila ifikapo wiki ya mwisho ya mwezi Novemba kote Duniani.
Akizungumza katika zoezi hilo Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga amesema, wamehamasika kufanya zoezi hilo kwa lengo la kusafisha mazingira ya fukwe hizo ambazo zinakabiriwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kila siku.
“hii ni hamasa kwa wananchi na kuwakumbusha kuwa tunapaswa kuyalinda na kuyatunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye”
Kiwanga ameongeza kuwa mazingira ya bahari yanapaswa kulindwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha athari kwa mazao na viumbe bahari ambavyo ni muhimu kwa matumizi ya binadamu ikiwemo chakula, pia amewakumbusha watanzania kuwa na mwamko wa kupanda miti ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na ukame unaosababishwa na ukataji miti holela.
“kwa mfano mwaka huu, kuna changamoto ya kukosekana mvua za kutosha, hii yote ni inatokana na mwamko mdogo wa elimu ya utunzaji mazingira’’. Amesema kiwanga.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga ameongoza zoezi la upandaji miti katika eneo linalozunguka barabara na ufukwe wa msasani sanjari na ugawaji vyeti kwa wanafunzi 25 waliohitimu mafunzo ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira kutoka taasisi ya mazingira ya ECCT.
Zoezi hilo limewashirikisha pia viongozi wa serikali ya mtaa wa Bonde la mpunga kata ya Msasani, ambapo mwenyekiti wa mtaa huo Hemedi Chamwana ameushukuru uongozi wa FCS, Nipe fagio na ECCT kwa kusirikiana na wananchi wa eneo hilo kwa kufanya usafi, kupanda miti pamoja na kutoa hamasa na elimu ya utunzaji wa mazingira.
Aidha Afisa wa masuala ya kijamii wa taasisi ya ECCT Desderi Msafiri ametoa wito kwa wazalizaji wa bidhaa za viwandani kama vile vifungashio vya bidhaa mbalimbali kushirikiana na wananchi katika suala zima la utunzaji wa mazigira kwa kuweka vifaa maalumu vya kuhifadhia taka katika maeneo hayo na kote nchini.
Maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika hufanyika kila mwaka ifikapo Disemba 9 tangu kuasisiwa kwake mwaka 1961. Kufuatia maadhimisho hayo, FCS imeihasa jamii kuwa na utamaduni wa kutumia siku za kitaifa kujitoa kwa kufanya kazi mbalimbali za kijamii katika maeneo yanayowazunguka.
PICHA MBALIMBALI ZA WANANCHI NA WATUMISHI WA FCS, NIPE FAGIO NA ECCT KATIKA ZOEZI LA USAFI