Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa AfroNet, Constatine Akitanda akitoa neno la ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kilimo wanaokutana nchini Kenya kujadili bidhaa na mazao ya GMO (1) Mratibu wa BIBA Kenya Anne Maina akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa kilimo unaofanyika nchini humo, kuhusu mazao na bidhaa za GMO Mratibu wa TABIO Tanzania, Abdallah Mkindi akitoa mada kuhusu GMO,mbele ya wadau wa kilimo wanaokutana nchini Kenya kwa siku mbili kujadili mazao na bidhaa hizo.
Mratibu wa TABIO Tanzania, Abdallah Mkindi akiwasilisha mada kuhusu GMO,mbele ya wadau wa kilimo wanaokutana nchini Kenya kwa siku mbili kujadili mazao na bidhaa hizo.
********************
Na Selemani Msuya, Nairobi
WADAU wa kilimo kutoka nchi za Kenya, Tanzania na Uganda wametakiwa kushirikiana, ili kuzuia uingizaji na Bidhaa na Mbegu zinazotokana na Vinasaba vya (GMO) katika nchi zao na Afrika Mashariki.
Wadau hao wamesema hayo katika mkutano unaofanyika katika eneo la Mto Athi, Machakos jijini Nairobi nchini Kenya kwa kuratibiwa na Taasisi ya Bioanuai na Usalama ya Kenya (BIBA) Shirika lisilo la Kiserikali Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO) na Participatory Ecological Land Use Management (PELUM Uganda).
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kuendeleza Kilimohai Barani Afrika (AfrONet) Constantine Akitanda, amesema Afrika ipo katika hatari ya usalama wa chakula, iwapo mazao na bidhaa za GMO zitaruhisiwa kuzalishwa au kuingizwa, hivyo ni jukumu la kila Mwafrika hasa mkulima mdogo kushiriki mapambano kuzuia.
“Katika kukabiliana na GMO sisi wadau wa kilimo tunapaswa kushikamana na kupinga bidhaa na mazao hayo kwani sio salama, sisi AfroNet tumejipanga kutoa ushirikiano pale ambapo tutahitajika,” amesema.
Akitanda amesema mkutano huu ambao umekutananisha wadau wa kilimo wa nchi za Kenya, Tanzania na Uganda ni hatua muhimu ya kufanikisha mapambano hayo.
“Afrika ipo katika hatari kubwa ya kuwa uwanja wa kutupia bidhaa za GMOs kutoka kwenye sekta ya kubadili vinasaba na maabara kutoka kwa wana sayansi wenye uchu wa kujinufaisha binafsi huku wakiwaondosha wakulima wadogo kwenye kilimo.
Wanasayansi hao pamoja na mtandao wao mkubwa duniani wanasambaza jumbe zenye maneno matamu mazao yaliyobadilishwa vinasaba yataleta ukombozi na kwamba ni suluhu kubwa katika kutokomeza njaa, lakini ukweli ni kwamba GMOs itaongeza matatizo ya upatikanaji wa chakula Afrika na kuongeza umasikini,” amesema.
Amesema mtazamo wa taasisi AfrONet ni kwamba Waafrika wanaouwezo mkubwa wa kuzalisha kwa kutumia mbegu zao na teknolojia rafiki kwa mazingira na usalama wa chakula kinachozalishwa pamoja na afya za walaji kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima Wadogo Kenya, Justus Mwololo amesema mkutano huu umesubiriwa kwa muda mrefu, hivyo ni jambo la kupongeza kwa kufanikiwa kufanyika, hivyo anatarajia washiriki wataeleza mambo ambayo yanaenda kuleta mapinduzi katika eneo hilo.
Mjumbe huyo wa Bodi ya BIBA, amesema hatua ya mahakama kuu ya Kenya kuzuia uingizaji na usambazaji wa bidhaa za GMO hadi hukumu ya kesi iliyofunguliwa isikilizwe ni wa kuungwa mkono na kila mdau wa kilimo Afrika.
“Ni wakati muafaka wa sisi wakulima wa Afrika Mashariki kuja na mkakati wa pamoja ambao utayafanya mazao ya GMO na bidhaa zake hayapati nafasi. Na hili linaweza kufanikiwa iwapo tutaweka mkazo katika vyombo vyenye maamuzi kama Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN),” amesema.
Mwololo amesema pia ni wakati muafaka wa kuwa na mkakati wa kilimo hai ambacho kitaondoa changamoto ya chakula kwa wakulima, ili wasiweze kushawishiwa kushiriki kilimo cha GMO.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kilimo Ikolojia na Kamati ya Kitaifa ya Uganda (EOAI-NSC), Dk Murongo Flarian amesema kupitia mkutano huo wa siku mbili watafanikiwa kujadiliana namna ya kuondoa vikwazo katika sekta ya kilimo kwa nchi zao.
“Tunatakiwa tutumie mkutano huu kujadili kwa kina kuhusu GMO na kilimo hai, ili tuweze kwenda na msimamo mmoja ambao ni endelevu kwao,” amesema.