Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza James Ruge akitoa taarifa ya ufuatiliaji wa miradi 27 inayoendelea kutekelezwa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza James Ruge akitoa taarifa ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa waandishi wa habari
**************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza kupitia dawati la uzuiaji rushwa imefuatilia utekelezaji wa miradi 27 yenye thamani ya Sh.Bilion 16.2 kwa kipindi cha Julai-Septemba 2022.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Disemba 8, 2022 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza James Ruge, wakati akitoa taarifa ya ufuatiliaji wa miradi hiyo kwa waandishi wa habari.
Akitoa mchanganuo wa miradi hiyo Ruge ameeleza kuwa Nyamagana ni miradi 14 ambapo miradi 11 ni ya afya na mitatu ya elimu, Ilemela miradi 2,Magu 3, Ukerewe 2,Sengerema 2,Misungwi 2 na Kwimba 2.
Amesema miradi yote 27 inaendelea na iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji huku akielezea baadhi ya miradi kuwa na dosari ikiwemo ya ucheleweshwaji wa vifaa tiba kwenye miradi 10 katika taasisi ya tiba Bugando inayotekelezwa chini ya mpango wa UVIKO 19.
Ruge ameeleza miradi 3 ya ujenzi wa matundu ya vyoo,ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari Nyamagana pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) Hospitali ya Fumagila Nyamagana inayofadhiliwa na TASAF kulikuwepo na changamoto ya kufungwa kwa mfumo wa malipo ushauri ulitolewa na changamoto hiyo ilitatuliwa na miradi inaendelea.
” Moja ya kazi za TAKUKURU kupitia jukumu lake la kuzuia rushwa nchini ni kufanya udhibiti wa mianya ya rushwa kwenye taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kwa kuchambua mifumo ya utendaji kazi kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa ili kutoa ushauri wa namna bora ya kutoa huduma na kuepuka vitendo vya rushwa”, amesema Ruge
Amesema kipindi cha Julai-Septemba mwaka huu jumla ya chambuzi sita za mfumo zimefanyika katika sekta ya mapato,maji,usafirishaji,madini,ujenzi na biashara
” Kwenye chambuzi hizo TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imefanya udhibiti na kuziba mianya ya rushwa kwenye ukusanyaji wa ushuru wa madini ujenzi ambapo jitihada hizo zimezaa matunda na Halmashauri ya Misungwi,Kwimba na Sengerema zimefanikiwa kukusanya mapato zaidi ya milioni 4″, amesema Ruge