Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Taifa ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akifungua Mkutano wa 10 wa Chama cha Mapinduzi CCM uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 07 Desemba, 2022.
Viongozi, wageni mbalimbali kutoka Vyama Rafiki pamoja na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 07 Desemba, 2022.
****************
Alex Sonna_DODOMA
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) taifa, Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo chama hicho kimedhamiria kufanya mageuzi ya kukirudisha chama mikononi mwa wanachama.
Akifungua leo Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM jijini Dodoma, Rais Samia amesema miongoni mwa mikakati yake ni kupanua wigo wa demokrasia na nafasi za uongozi ndani ya chama kwa kufanya marekebisho ya katiba kwa kuongeza viti vya Ujumbe wa Halmashauri Kuu wa CCM(NEC).
“Katika kupanua wigo na ushiriki wa wanachama katika kufanikisha jukumu la kutafuta ushindi wa chama kwenye chaguzi, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeamua kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya katiba ili kuongeza nafasi za wajumbe wa NEC kutoka viti 15 hadi 20 kwa kila upande Tanzania bara na Zanzibar,”amesema.
Aidha, amesema pia kuongeza wajumbe wa NEC wanaopatikana kwa kuteuliwa kutoka saba hadi 10.
“Ni matarajio yangu wakati utakapofika kila mmoja wetu na hususan wajumbe wa mkutano mkuu tutazingatia kwa makini mapendekezo hayo na kupitisha kwa faida na maendeleo ya chama chetu na Tanzania kwa ujumla,”amesema.
Akizungumzia kuhusu dhumuni la mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amesema mkutano huo unahitimisha zoezi la uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya wa mwaka 2022.
“Hivyo kwa kuzingatia ibara ya 100 mkutano huo unatakiwa kutekeleza mambo matatu ambayo ni kufanya marekebisho ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022,”amesema.
Aidha, amesema “Kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM, serikali za pande mbili na taarifa ya Halmashauri kuu ya ccm Taifa juu utekelezaji wa kazi za chama na jumuiya zake kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.”
“Pia, uchaguzi wa viongozi wa CCM ngazi ya taifa ambao ni wajumbe wa Halmshauri Kuu Taifa viti vya taifa kundi la Bara na Zanzibar, Makamu Mwenyekiti Zanzibar na Bara na Mwenyekiti wa CCM Taifa.
“Ndio maana kauli mbiu yetu inasema CCM imetimia baada ya mkutano wa leo ni kazi kusonga mbele, kwa niaba ya kamati tendaji ya mandalizi ya mkutano mkuu huu nawahakikishia wajumbe maandalizi muhimu yote ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi yamekamilika na natumaini mtatimiza wajibu wenu kwa weledi na kwa mafanikio makubwa,”amesema Chongolo.
Awali amesema kuwa jumla ya wanachama walioomba kuteuliwa kugombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya shina ni milioni 1.213, matawi ni 674,624, kata na ward kwa Zanzibar 187, 873, wilaya 24,439, mkoa 1,568 na taifa 2,799 kuomba nafasi ya viti 30 ambapo 15 Bara na 15 Zanzibar vya halmashauri kuu vya CCM Taifa .