****************
Mwandishi wetu, Babati
TIMU ya soka ya Makilayoni FC imetwaa ubingwa wa michuano ya Chem chem CUF 2022 baada ya kuichabanga timu ya Mdori FC kwa penati 4-2 katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Mdori Wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.
Katika mchezo huo, ambao mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa mkoa Manyara, Charles Makongoro Nyerere hadi dakika 90 zilipomalizika timu hizo zilitoka sare kwa kufungana 1-1.
Baada ya ushindi huo mabingwa hao ambao wametwaa mara mbili mfululizo mwaka2021 na 2022 walipewa zawadi ya fedha taslim sh 1 milioni, kombe lenye thamani ya sh 1 milioni na Mpira.
Katika michuano hiyo ambayo mwaka huu lengo lilikiwa ni kupiga vita ujangili wa Twiga jumla ya timu 16 zilishiriki kutoka katika vijiji 10 ambavyo vinaunda Jumuiya ya Hifadhi ya wanyamapori ya Burunge (JUHIBU).
Mdori FC wakipewa zawadi ya Kombe na fedha taslim shilingi 500,000 mpira ambapo awali timu zote 16 zilipewa seti ya jezi na mpira ili kushiriki michuano hiyo ikiwepo timu za mpira wa Pete..
Akizungumza katika michuano hiyo, Mkuu wa mkoa Manyara Makongoro Nyerere amewataka vijana kushiriki katika kupambana na ujangili na kutunza mazingira.
“Michezo hii sio tu ni fursa ya kukuza vipaji na kupata burudani lakini inalenga vijana kupambana na ujangili lakini pia kuhifadhi mazingira,” amesema.
Meneja mahusiano wa taasisi ya Chemchem, Charles Sylvester ambayo imewekeza shughuli za Utalii wa picha na hoteli katika eneo hilo la JUHIBU amesema michuano hiyo tangu imeanzishwa miaka 10 iliyopita imekuwa na faida kubwa.
“Tumepata vipaji kuna wachezaji wametoka hapa wameenda ligi kuu lakini pia vijana wengi wamekuwa malinzi wa Wanyamapori na kupenda uhifadhi na tutaendelea kuiboresha,” amesema.
Mwenyekiti wa michuano hiyo, Belela Erasto amesema michuano ya mwaka huu imegharimu zaidi ya million 50 alipongeza wawekezaji ya Chemchem kwa kuendelea kudhamini michuano hiyo kila mwaka.
Erasto amesema hao waliowekeza hoteli za kitalii na Kitalu Cha Uwindaji kupitia kampuni tangu za EBN na kufanya Utalii wa picha wamekuwa na manufaa makubwa katika wilaya ya Babati na mkoa mzima wa Manyara ikiwepo kutoa ajira zaidi ya 300, ujenzi wa shule, kusaidia sekta ya afya, maji na vikundi vya wanawake