Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kamishna Jenerali Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 7,2022 katika Ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kamishna Jenerali Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 7,2022 katika Ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.
****************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilo 16.643 za dawa za kulevya zikijumuisha kilo 15.19 za heroin, gramu 655.73 za Cocaine na gramu 968.67 za Methamphetamine zilizowahusisha jumla ya watuhumiwa saba.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 7,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kamishna Jenerali Gerald Kusaya amesema ukamataji wa kilo 15.19 za dawa za kulevya aina ya heroin zilizowahusisha watuhumiwa watatu ni mwendelezo wa operesheni zilizopita.
” Watuhumiwa hawa ni Washirika wa Kambi Zuberi Seif na wenzake waliokamatwa wakiwa na kilo 34.89 za heroin katika operasheni ya mwanzoni mwa mwezi Novemba 2022″. Amesema Kamishna Jenerali Kusaya.
Aidha amesema watuhumiwa hao watatu ni Suleiman Thabiti Ngulangwa (36), mfanyabiashara na mkazi wa Salasala, Sharifa Seleman Bakar(41), Mkazi wa Maji matitu-Mbagala , wote ni wakazi wa Dar es Salaam.
Hata hivyo amesema watuhumiwa wengine wanne walikamatwa wakiwa na gramu 655.75 za cocaine na gramu 968.67 za Methamphetamine.
Amesema watuhumiwa walikamatwa wakiwa kwenye harakati za kusafirisha dawa hizo za kulevya kwenda nje ya nchi.
“Watuhumiwa hao wanne ni Hussein Rajab Mtitu (28)anayejulikana pia kama Chodri Mohamed mfanyabiashara na mkazi wa Kibonde Maji, Mbagala , Jaalina Rajab Chuma (31) anayejulikana pia kama Jaalina Mohan mjasiriamali na mkazi wa Tandika, Shabani Abdallah Said (36) mkazi wa Kilimahewa, Tandika, hawa pia ni wakazi wa Dar es Salaam pamoja na Irene Dickson Mseluka (39) mfanyabiashara na mkazi wa Ndala Shinyanga”. Amesema