Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema akionesha miongozo mitatu ya elimu baada ya kuizindua katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenye hafla iliyofanyika katika kumbu wa sekondari ya Songea Girls ikishirikisha wadau mbalimbali wa elimu
baadhi ya wadau wa elimu kutoka Manispaa ya Songea wakishiriki kwenye hafla ya uznduzi wa miongozo mitatu ya elimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea
………………………………
Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mheshimiwa pololet Mgema amezindua miongozo mitatu ya usimamizi na uendeshaji wa elimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa na wadau wa elimu kutoka Manispaa ya Songea na kufanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Songea Girls mjini Songea.
Akizungumza kabla ya kuzindua miongozo hiyo Mkuu wa Wilaya amesema uzinduzi huo wa miongozo ya elimu ni muendelezo wa utekelezaji wa uzinduzi wa kitaifa uliofanywa na Waziri Mkuu na uzinduzi wa kimkoa uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Amesema ili miongozo hiyo iweze kuleta ufanisi,inafaa ieleweke vizuri kwa wadau wote wa elimu katika ngazi ya shule na ngazi ya jamii na kwamba miongozo imeanisha masuala mbalimbali ya elimu ikiwemo changamoto za kielimu na utatuzi wake katika shule za msingi na sekondari.
“Changamoto kubwa zinazotakiwa kufanyiwa kazi ni udhibiti wa utoro wa wanafunzi,Mkuu wa shule ahakikisha wanafunzi wanaitwa majina mara mbili kwa siku ili kujua kama kuna watoro ,pia mzazi aitwe shuleni iwapo mtoto wake hatahudhuria shule siku mbili mfululizo’’,alisisitiza.
Mkuu wa wilaya pia amewaagiza wadau wa elimu kutafutia ufumbuzi changamoto ya ukosefu wa chakula shuleni,amemwagiza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea,kuangalia uwezekano wa kutunga sheria zinazowabana wazazi ambao hawataki kuchangia chakula kwa Watoto wao na kwamba agenda ya chakula iwe ya kudumu kwenye vikao.
Katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya pia aliagiza wadau wa elimu kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu,ikiwemo upungufu wa samani,vyoo,vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu na kutoa mafunzo kazini kwa walimu.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Alto Liwolelu aliitaja miongozo mitatu ambayo imezinduliwa kuwa ni Mwongozo ambao umeainisha changamoto katika elimu ya msingi na sekondari.
Ameutaja mwongozo wa pili kuwa unahusu mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya msingi na mwongozo wa tatu umeeleza kuhusu uteuzi wa viongozi wa elimu katika mamlaka za serikali za mitaa na mikoa.
Hata hivyo amesema miongozo yote mitatu imebeba changamoto na taratibu za usimamizi na uendeshaji wa elimu ya msingi na sekondari na kwamba miongozo hiyo inakusudia kuleta tija katika sekta ya elimu kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Michael Mbano amewaagiza walimu wakuu kuhakikisha katika shule zao wanapanda miti ikiwemo miti ya matunda ili kuhifadhi mazingira katika shule zao.
Kuhusu upatikanaji wa chakula shuleni,Mbano amesema watafanya mikutano na wazazi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuchangia chakula kwa Watoto wao wanapokuwa shuleni.
Naye Afisa Elimu Shule za Msingi Katika Manispaa ya Songea Frank Sichalwe akizungumzia kwa ujumla changamoto za walimu,amekiri kwenye Halmashauri za Manispaa,miji na majiji hakuna mwalimu anayehamia,pia katika Halmashauri hizo hakuna ajira mpya za walimu.
“Tuna uhaba mkubwa wa walimu,wakati huo huo walimu walio wengi wanastaafu kwa hiyo katika Manispaa ya Songea hakuna shule hata moja yenye mwalimu wa ziada’’,alisisitiza Sichalwe.
Kuhusu upatikanaji wa miundombinu katika shule za msingi,Sichalwe amesema anaishukuru serikali ambayo hivi sasa inajenga madarasa mengi katika shule za msingi hivyo kupunguza uhaba wa miundombinu ya madarasa katika manispaa ya Songea.
Hata hivyo amesema baada ya serikali kutoa miongozi hiyo mitatu ya elimu,Manispaa ya Songea inakwenda kutafutia ufumbuzi changamoto hiyo ya uhaba wa walimu na changamoto nyingine ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
Miongozo hiyo mitatu ya usimamizi wa elimu imeundwa Julai mwaka huu kupitia Wizara ya TAMISEMI ikiwa ni juhudi za serikali ya awamu ya sita kuboresha elimu ili wananchi wake wapate elimu bora na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Tanzania.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma