WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro,akizungumza na waandishi wa habari wakati akifungua maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa 2022 yaliyoanza leo Disemba 6,2022 jijini Dodoma.
……………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amewaonya Watumishi wa umma wanaoendekeza Vitendo vya Rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao hususani katika kuwahudumia wananchi.
Onyo hilo amelitoa leo wakati akifungua maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa 2022 yaliyoanza leo Disemba 6 jijini Dodoma.
Dkt.Ndumbaro amesema kuwa tayari wameweka mifumo madhubuti ya kuwanasa wote wanaopokea na kutoa rushwa katika kuhudumia wananchi.
“Nimeeleza hapo juu kwamba siku ya Maadili na Haki za Binadamu tunayoadhimisha kila mwaka hapa nchini, imetokana na siku mbili tofauti ambazo huaadhimishwa kimataifa ambazo ni siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa pamoja na Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.
“Rushwa ni tatizo katika nchi nyingi duniani hivyo mwaka 2003, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilikubaliana kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa kila tarehe 9 Desemba kuanzia mwaka 2004 ikiwa ni fursa mojawapo kwa kila nchi kutathmini juhudi zake za kudhibiti vitendo vya rushwa”amesema Dkt.Ndumbaro
Amesema kuwa vita ya Rushwa bado ni kubwa hivyo wanahabari wanalojukumu la kutumia vizuri kalamu zao katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kushiriki kwa vitendo katika kuikataa na kufichua vitendo vya rushwa.