*************************
Na WAF, Dar Es salaam.
Matumizi ya dawa za muda mfupi ambayo ni mchanganyiko wa dawa mbili (Isoniazid na Rifampicin) zitasaidia sana kupunguza watu kuugua kifua kikuu nchini.
Hayo yamesemwa na Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini Dkt. Riziki Kisonga katika hafla ya kutangaza matokeo ya ufuasi wa Dawa za Kifua Kikuu (TB) kupitia mradi wa ASCENT – KNCV.
Dkt. Kisonga amesema ili tuweze kupunguza ugonjwa wa kifua kikuu usiweze kuongezeka na kusambaa kwa watu wengine lazima tuzuie wale ambao wana hatari ya kupata ugonjwa huo wasiambukizwe.
“Makundi yaliyo katika hatari ya kuugua ugonjwa huu ni pamoja na watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, wanaotumia dawa za kulevya na makundi ya watu wanaofanya shughuli za uchimbaji, wazee, na watu wanaoishi na wagonjwa wa Kifua Kikuu” amesema Dkt. Kisonga
Pia Dkt. Kisonga amesema dawa hizo tumekuwa tukizitumia nchini hazina madhara makubwa na matumizi yake zitakuwa zinatumika mara moja kwa wiki kwa muda wa miezi mitatu badala ya kutumia kila siku kwa muda wa miezi sita
Aidha,Dkt Kisonga ametoa rai kwa jamii kuhamasika pale ambapo nchi itaanzisha matumizi ya dawa hizo, lengo kubwa ni kuhakikisha tunapunguza ugonjwa wa Kifua Kikuu kwani huwezi kuuondoa ugonjwa huo kama hutakuwa na njia mbalimbali za kuutibu.
Kwa upande wake meneja mradi wa ASCENT – KNCV Bw. Baraka Onjare amesema teknolojia ya ufuasi wa dawa imeleta matokeo makubwa kwa kupunguza wagonjwa wanao toroka matibabu mwanzoni.
“Box hizi za smart pill zina leta mawasiliano ya karibu kati ya mtoa huduma na mgonjwa kitu ambacho kina ongeza ufuatiliaji wa wagonjwa, pia tumeona wateja wamependa teknolojia hii kwani ina wakumbusha muda wa kunywa dawa kwa njia ya alamu na meseji” amesema Bw. Onjare