Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa BASATA Dkt. Kedmon Mapana amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa nafasi na fursa nyingi kwa sekta za utamaduni na sanaa ambazo zimeweza kutoa ajira kwa vijana wengi kwa wakati mmoja.
Hayo ameyasema wakati akifungua kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa Tamasha la Utoaji Tuzo la Uni Awards msimu wa nne 2022 leo Desemba 4, 2022 katika ukumbi wa JNICC Dar es salaam.
Amesema kuwa tasnia imewekewa mazingira mazuri kuanzia kwa Mhe Rais wa awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Wizara hivyo ni wakati sahihi kwa kufanya uwekezaji kwenye sekta ya sanaa ili kukuza uchumi na Serikali imeahidi kuwa sambamba ili Uni Awards iwe ya kimataifa.
Ameongeza kuwa sekta hii imethibitika kuongeza pato la nchi kwa asilimia 19 hivyo haipaswi kubezwa isipokuwa kutiliwa mkazo katika ubunifu kwakuwa inaaminika Tanzania itakuwa maradufu kisanaa baada ya Nigeria kwa sasa.
Juu ya hapo amewatia moyo wanachuo kuwa sanaa ya nchi imezidi kushika kasi katika majukwaa ya kimataifa akitolea mfano Tuzo ya Afrimma aliyokabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakati huohuo, mratibu wa tuzo hizo Bi. Shine Basil ameishukuru Serikali kwa namna inavyojitoa kuhakikisha tamasha linafanyika na kwakuwa linakutanisha vijana kutoka vyuo mbalimbali hivyo linawajengea msingi imara wa kutambua ajira katika sekta ya Sanaa.