MAANDAMANO wakati wa Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha St.John’s Tanzania yaliyofanyika jijini Dodoma ambapo wahitimu 965 walitunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali ya elimu na Mkuu wa Chuo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Donald Mtetemela.
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha St.John’s Tanzania, Prof.Yohana Msanjila,akizungumza wakati wa Mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dodoma ambapo wahitimu 965 walitunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali ya elimu na Mkuu wa Chuo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Donald Mtetemela.
MWENYEKITI wa Baraza la Chuo Kikuu cha St.John’s Tanzania,Prof.Penina Mlama,,akizungumza wakati wa Mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya wahitimu wa kada mbalimbali wakiwa katika hafla ya mahafali ya 36 ya Chuo Kikuu cha St.John’s Tanzania, yaliyofanyika chuoni hapo, jijini Dodoma.
Mhitimu Emanuel Kombe,akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake katika hafla ya mahafali ya 36 ya Chuo Kikuu cha St.John’s Tanzania, yaliyofanyika chuoni hapo, jijini Dodoma.
…………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha St.John’s Tanzania,wametakiwa kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kujiajiri badala ya kutegemea ajira rasmi pekee ili kujikwamua kimaisha.
Hayo yamesema Mwisho Mwa wiki Jijini Dodoma na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof.Yohana Msanjila,kwenye mahafali ya 13 ya chuo hicho ambayo wahitimu 965 wametunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali ya elimu na Mkuu wa Chuo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Donald Mtetemela.
Prof.Msanjila aliwataka wahitimu hao kuitumikia jamii kwa uaminifu kama sehemu ya programu zao za mafunzo walizofundishwa kwa kuzifanyia upembuzi yakinifu,ili kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii na kuleta mabadiliko chanya.
“Muwe mabalozi wazuri wa chuo chetu huko muendako kumbukeni kwamba popote muendako mmebeba nembo na kauli mbiu ya chuo kwenda kutumika kwa weledi na uaminifu mkubwa,mtumie maarifa mliyopata kujiajiri na kuajiriwa,”alisema Prof.Msanjila
Aidha Prof.Msanjila alisema kuwa elimu waliyoipata itakuwa na thamani kubwa endapo itaendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika kuleta suluhisho la kero zinazoikabili nchi.
Alisema chuo hicho kimeendelea na uboreshaji wa mitaala ikiwa ni pamoja na kuongeza kozi mpya ambazo mbili zinasubili kibali kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kabla ya kuanza kutumika.
“Chuo kinakusudia kuanzisha kozi fupi kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo huduma kwa wateja, ujasiriamali na utafutaji wa masoko ya bidhaa, zitatolewa kwa watumishi wa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, na watu binafsi watakaopenda,”alisema.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utendaji kwake ambao chuo kina imani naye sambamba na uwekezaji unaofanyika na uimarishaji wa diplomasia ya kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Prof.Penina Mlama, alisema taasisi za vyuo vikuu huandaa watalaamu mbalimbali ikiwamo afya, kilimo, biashara, uhandisi na kupitia hao nchi inapata mafanikio kadhaa.
“Sisi ni wadau muhimu wa elimu, mchango wa wahadhiri umesaidia kuboresha hali za watanzania popote nchini kupitia kazi zenu mmefungua fursa nyingi kwa wadau, naomba muendelee na juhudi hizi ili nchi yetu iendelee kupaa kielimu na kiuchumi,”alisema.
Naye Mhitimu Emanuel Kombe, aliwaomba wahitimu kutumia elimu na maarifa waliyoyapata kujikwamua kiuchumi kutokana na nchi kukabiliwa na tatizo la ajira.