**************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayesimaia Sekta ya Uchukuzi Bw. Gabriel Migire amesema Kufikia Januari, 2023 Bandari kavu ya Kwala iliyopo Mkoani Pwani itaanza kupokea Mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam.
Migire ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa Barabara yenye urefu wa kilometa 15 kutoka Vigwaza mpaka Bandari Kavu ya kwala inayojengwa kwa kiwango cha Zege na Kampuni ya Stem kutoka Jijini Dar es salaam na kusimamiwa na wakala wa Barabara hapa nchini ( TANROADS) ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika Desemba 30,2023.
“ Kuanza kutumika kwa Bandari hii ya Kwala itasidia kupunguza Msongamano wa Mizigo na magari makubwa katika Bandari ya Dar es salaa, Bandari hii ya Kwala itahifadhi Makasha ya kwenda nchi Jirani kama vile Burundi, Rwanda, DRC Congo, Uganda , Zambia na Malawi “ amesema Migire.
Kwa upende wake Mhandisi Joseph Marandu kutoka SUMA JKT anayesimamia Ujenzi wa Bandari ya Kwala amesema kuwa ujenzi upo katika hatua nzuri na wanatarajia kukamilisha ujenzi Desemba 30, 2022 kwa sasa wanaendelea na kazi ya kuweka Taa , Kamera Pamoja na kumalizia kuweka Sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia Makasha.
Naye Mhandisi Jacob Mambo kutoka wakala wa Barabara hapa nchini(TANROADS) anayesimamia Ujenzi wa Barabara hiyo kutoka vigwaza mpaka Bandari Kavu ya Kwala amesema kuwa ujenzi wa Barabara umekamilika, kazi zilizobaki ni kuweka alama za barabarani Pamoja na Mzunguko eneo la Vigwaza ambapo kazi hiyo inatarajia kukamilika Disemba 7 mwaka huu.
Lilian Molel Pamoja na Baton Mwaselela ni wananchi wanoishi karibu na Bandari kavu Kwala ,wamesema kuwa ujenzi wa Bandari hiyo umeanza kusaidia vijana wengi wa eneo hilo kupata ajira za kudumu na ajira za Muda hivyo wanategemea kupata maendeleo ya kijamii na kuongeza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa mustakabali wa maendeleo ya eneo la Kwala na Mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Bandari ya Kwala inategemewa kupunguza foleni ya magari Makubwa katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa mizigo mingi itasafirishwa na treni kutoka Bandari ya Dar es salaam na kupelekwa Kwala na hapo ndipo magari makubwa yatakuwa yanachukulia mizigo yake. Tayari miundombinu muhimu kama vile Barabara, Umeme, Maji Pamoja na Reli vimeshajengwa katika Bandari hiyo.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini wizara ya Ujenzi na Uchukuzi