Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Masoud Othman akipata maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru Dauson Malela ya namna bunifu bora na ya kipekee ya zana rahisi ya kupandia pamba maarufu ‘Rafiki Planter’ inavyofanya kazi. Tukio hilo lilitokea kwenye Maonesho ya Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru na Mratibu wa zao la pamba Tanzania Dk. Paul Saidia akielezea sababu zilizopelekea watafiti wa kituo hicho kubuni teknolojia hiyo rahisi na rafiki ya kupandia pamba maarufu ‘rafiki planter.’
Mtaalamu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru Dauson Malela akionyesha zana hiyo waandishi wa habari waliofika kituoni hapo (hawapo pichani)
Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.
Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.
Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.
Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.
Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.
Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani
Kabla ya ugunduzi wa zana hiyo hali halisi ni kama inavyoonekana pichani kwa wakulima wa pamba kutumia muda mrefu kutengeneza kamba, kunyoosha mstari, kuweka alama na vipimo, kuchimba mashimo, kudondosha mbegu na kuzifukia kwa kutumia jembe la mkono jambo lililopelekea vijana wengi, wanawake na wazee kukata tamaa na kutafuta shughuli nyingine. Hivyo bunifu hiyo sasa ni mwarobaini wa changamoto hizo.
Na Godwin Myovela
WATAFITI kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru wapo kwenye
mchakato wa maboresho ya bunifu yao ya zana rahisi na ya kipekee ya kupandia
pamba maarufu ‘Rafiki Planter’ kutoka hatua ya kukokotwa na wanyama na kuvutwa
na binadamu na sasa kuwekewa viongeza mwendo (motorised machines) ili kuongeza
ufanisi.
Zana hiyo ambayo imegeuka mkombozi kwa wakulima wa pamba kwa kurahisisha
shughuli zote za upandaji, ina uwezo wa kutumia kati ya saa moja mpaka masaa 3
kupanda eneo la ekari moja, ikilinganishwa na wastani wa masaa kati ya 10 na 11
ambayo hutumika kama zao hilo litapandwa kwa mkono.
Aidha, zana hiyo inapokuwa inakokotwa au kuvutwa na binadamu kupitia sehemu
maalum ya kufunga mnyororo au mkono wake
wa kuvuta, ina uwezo wa kudondosha mbegu kutoka shimo hadi shimo kwa cm 30, na
kutoka mstari hadi mstari cm 60, sanjari na uwezo wa kubeba mbegu kati ya kilo
3 mpaka 6 kupitia vibeba mbegu maalum
kwa wakati mmoja.
Pia ugunduzi huo, umeiwezesha zana hiyo kuwa na uwezo mahsusi ya
kutengeneza yenyewe mashimo ya mbegu na vifukia udongo ambavyo hufanya kazi
yake punde tu mbegu inapodondoshwa.
Kwa mujibu wa Tari, teknolojia ya zana hiyo imewekewa mfumo wa vifungua
ardhi ambavyo kadiri zana hiyo itakavyokuwa inasogea vifungua ardhi hivyo
vinachimba mashimo kwa maana ya
kutengeneza mifereji kwa umbali wa cm 60 kutoka kimoja hadi kingine.
Mkurugenzi wa kituo hicho, ambaye pia ni mratibu wa zao la pamba nchini,
Dk. Paul Saidia alisema ugunduzi huo na maboresho yake vitahusisha, kushawishi
na kuvutia idadi kubwa ya makundi mbalimbali wakiwemo vijana, wanawake na wazee
kuingia katika kilimo tofauti na ilivyokuwa awali, na hivyo kuongeza tija zaidi
ya mara mbili kwenye uzalishaji wa pamba.
Akizungumza jijini hapa, wakati akishiriki utekelezaji wa mradi wa kuinua
thamani kwenye mnyororo wa zao la pamba unaojulikana kama ‘Beyond Cotton,’
Saidia alisema kabla ya uwepo wa zana hiyo, na baada ya kufanya majaribio
walibaini nguvu kazi ya wakulima kati ya 12 na 14 ilitumika kupanda ekari moja
kwa siku 1 kwa wastani wa masaa 10 hadi 11.
Aidha, alisema hali hiyo hata hivyo ilipelekea usumbufu kwa wakulima walio
wengi kutumia muda mrefu kutengeneza kamba, kunyoosha mstari na kuweka vipimo
kwa kutumia zana duni za jembe la mkono sambamba na kuinama kwa muda mrefu,
hususan wakati wa kudondosha mbegu na kufukia, hali iliyosababisha ugumu kwenye
kufikia azma ya uzalishaji wa pamba kwa tija.
“Sasa naamini bunifu hii ni mkombozi
sababu inafanya kazi zote tatu; kwa maana ya kuchimba mashimo yenyewe,
kuweka mbegu na kufukia. Pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Tume
ya Sayansi Teknolojia Bodi ya Pamba nchini
tupo kwenye mchakato wa kuifanyia maboresho kwa kuifungia ‘motorised
machine’ itakayotumia mafuta ya petrol ili kuipa ufanisi zaidi,” alisema
Dk. Saidia.
Zaidi alisisitiza; “Kilichopelekea wazo la uvumbuzi huu ilikuwa ni
baada ya tafiti nyingi za kubadilisha namna ya upandaji pamba kutoka kwenye cm
90 kwa 40 wa hapo awali kuja kwenye huu mpya wa sasa wa cm 60 kwa 30 kufanywa kupitia mradi wa
‘Cotton Victoria’ katika azimio lililofanyika kwenye mkutano wa wadau mkoani
Simiyu mwaka 2020.”
Ikimbukwe, katika mkutano huo ilionekana upandaji mpya wa cm 60/30 pamoja
na uzuri wake lakini bado ulikuwa na changamoto ya matumizi makubwa ya muda,
ongezeko la nguvukazi na idadi ya mimea. Mathalani upandaji wa cm 90/40
ililazimika kuwa na mashimo yapatayo 11,111 kwa ekari, wakati 60/30 idadi ya
mashimo ya kupandia mbegu ni 22,222.
Kwa mantiki hiyo, kwenye kila shimo au mashimo zinapopandwa zaidi ya mbegu
2 kitaalamu inashauriwa mkulima ang’olee ili ibakie mimea 2; na kwa kufanya
hivyo, idadi ya upandaji wa awali wa cm 90/40 kwa mashimo 11,111 mimea itakuwa
22,222, na upandaji wa sasa ulioidhinishwa nao mimea itaongezeka mara mbili
zaidi kutoka 22,222 hadi idadi mpya ya 44, 444 kama itang’olewa na kubakizwa
miwili kwa kila shimo.
Kwa upande wake mmoja wa wataalamu kutoka Idara ya Uhaulishaji Teknolojia
ambaye pia ni miongoni watafiti wavumbuzi wa zana hiyo kutokaTari Ukiriguru,
Dauson Malela alipongeza Taasisi za Bodi ya Pamba nchini (TCB), Tume ya Sayansi
na Teknolojia (COSTECH) , Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini
(CAMARTEC) pamoja na kiwanda cha
kuchambulia pamba cha Biosustain mkoani Singida kwa ushirikiano mkubwa
walioutoa katika kufanikisha uvumbuzi wa zana hiyo.
Kwasasa Costech kwa kushirikiana na Tari wapo kwenye mchakato wa majaribio
kadhaa ya kuboresha zana hiyo kutoka kwenye mfumo wa sasa kwenda kwenye hatua
kubwa zaidi ya kufungia mashine itakayowezesha kujikokota yenyewe, ili hatimaye
iwe rahisi zaidi na rafiki kwa wakulima
wasio na mifugo na wazee wasioweza kuivuta.
Uvumbuzi wa zana hiyo unakwenda sambamba na falsafa ya sasa ya Wizara ya
Kilimo na Taasisi ya Utafiti nchini chini ya Waziri mwenye dhamana Hussein
Bashe ambaye mara kadhaa amekuwa akitoa maelekezo mahususi kwa wataalam wa
kilimo kuhakikisha wanaongeza kasi ya kiutendaji na tafiti ili kuleta mageuzi
chanya ndani ya sekta hiyo katika kufanikisha ajenda ya 10/30.
“Mchakato wa maboresho kwenye zana hii mali ya TARI ambayo
imegunduliwa na watafiti watatu Dk. Paul Saidia, Dauson Malela na Robert Chaleo
unaendelea, pia tunakaribisha wadau wengine kujitokeza ili kwa pamoja tuweze
kuinua tija ya kilimo cha pamba,” alisema Malela.