Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Itwelele iliyopo Manispaa ya Sumbawanga jana alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa .
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akizungumza na Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Lwiche. Kushoto ni Meya wa Manispaa hiyo Jastin Malisawa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akikagua majengo ya madarasa katika shule ya sekondari Kizwite jana ambapo alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo katika Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akisalimiana na walimu wa shule ya sekondari Kizitwe jana alipokwenda kukagu mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ambapo amewsihi waltumisha hao kuongeza jitihada za ufundishaji ili kukuza taaluma .
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Mtipe mjini Sumbawanga jana wakati alipokagua ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa kwenye shule hiyo .
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (katikati) akikagua miundombinu ya madarasa jana huku akiambatana na Maeya wa Sumbawanga Jastin Malisawa (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba (Kulia).
………………………………
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi vyumba Hamsini (50) vya madarasa kwenye shule za sekondari za Manispaa ya Sumbawanga kutokana na ubora na kasi ya ujenzi .
Ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya siku moja jana (Desemba 02,2022) aliyoifanya kukagua utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuongeza nafasi ya vyumba vya madarasa kwa ajili ya mapokezi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba, mkuu huyo wa mkoa alikagua maendeleo ya ujenzi kwenye shule za Itwelele, Lwiche, Kizwite, Kanda, Mazwi, Sumbawanga na Mhama ambapo madarasa hayo 50 yatakamilika Desemba 15 mwaka huu..
“Nimeridhishwa na namna kazi ilivyo nzuri ambapo nimeona mafundi na wasimamizi wakiwa kazini huku thamani ya fedha za serikali kwenye miradi hii ikiwa ikiaonekana tofauti na zamani” alisema Sendiga.
Sendiga akiongea na waandishi wa habari alisema ataendelea kuhakikisha halmashauri zinatekeleza miradi ya maendeleo kwa ubora na kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za umma na kuwa ataendelea kufuatilia bila kuchoka.
Serikali iliupatia mkoa huo shilingi 3, 820,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 191 za madarasa kwenye sekondari ili kumaliza tatizo la uhaba wa madarasa pamoja na madawati.
Mgawanyo wa vyumba vya madarasa hayo kwa kila halmashauri ni Manispaa ya Sumbawanga (56), Nkasi (26 ), Kalambo (63 ) na Sumbawanga DC ( 46) na kuwa madarasa hayo yatakamilika Desemba 15 mwaka huu .
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justin Malisawa alitoa wito kwa wazazi na walezi kujiandaa kuwapeleka shule watoto wao kwani serikali imeweka miundombinu karibu na maeneo yao na kuwa hakuna tena kikwazo kuhusu uhaba wa vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari.
Naye Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa Matinda Mwinuka alisema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa umefikia asilimia 73 kimkoa .