Na. Damian Kunambi, Njombe
Katika kuendeleza maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru hapa nchini ambayo huadhimishwa tarehe 9 Desemba kila mwaka hapa nchini, kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Ludewa Daniel Ngalupela kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Ludewa ameongoza zoezi la upandaji miti 61 ikiwa ni ishara ya kusherehekea miaka hiyo ya Uhuru.
Akizingua katika zoezi hilo akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi na serikali Ngalupela amesema miti hiyo ya matunda aina ya parachichi imepandwa katika eneo la ofisi ya mkuu wa Wilaya, kituo cha polisi Ludewa, shule ya sekondari Chief Kidulile pamoja na Gereza la wilaya ya Ludewa.
“Pamoja na kwamba tumepanda miti hii kwa kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru lakini pia ni sehemu mojawapo ya kuhamasisha wananchi katika upandaji miti yamatinda ili kuimarisha uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla”, Amesema Ngalupela.
Gervas Ndaki ni katibu wa CCM Wilaya ya Ludewa amesema katika kuadhimisha miaka hiyo 61 ya Uhuru watanzania wanapaswa kujivunia amani waliyonayo kwani katika kipindi chote tangu kupatikana kwa Uhuru hakujawahi tokea machafuko kama ilivyo kwa maeneo mengine.
Ameongeza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania awamu ya sita Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza amani waliyoiacha viongozi walipita na kusema kuwa amekuwa Rais aliye shupavu hivyo anastahili pongezi.