Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias amewataka wafanyabiashara wa soko la wilaya hiyo kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi kila ifikapo Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kutunza mazingira na kufanya biashara katika maeneo yaliyo safi.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo mara baada ya kuongoza zoezi la usafi sokoni hapo ikiwa ni ushiriki wa wiki ya maadhinisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania ambapo wilaya hiyo imeanza maadhimisho hayo tangu Desemba mosi kwa kufanya usafi maeneo mbalimbali kama sokoni, hospital na kwingineko.
“Nimezungunga eneo lote hili la soko lakini nimekuta kuna uchafu mwingi ikiwemo vinyesi hasa katika vyumba ambavyo havitumiki kitu ambacho ni hatari kwa afya zetu maana inaonekana kila mmoja hufanya usafi eneo analofanyia biashara pekee pasipo kujali maeneo mengine”, amesema Mkurugenzi.
Aidha kwa upande wake katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo Gervas Ndaki amese suala la usafi masokoni ni jambo la msingi kwani magonjwa mengi yanaotokana na ulaji chakula kichafu kama kipindu pindu huanzia masokoni.
” Msimu huu ni msimu wa mvua, maembe na vinginevyo ambavyo huenda sambamba na ugonjwa wa kipindupindu, hivyo endapo mtaacha taka hovyo kuna uwezekano mkubwa wa kutokea magonjwa ya mlipuko katika wilaya yetu”, amesema Ndaki.
Katika shughuli hiyo ya ufanyaji usafi sokoni hapo mkurugenzi Sunday Deogratias aliongozana na viongozi mbalimbali wa CCM pamoja na serikali huku wakiungwa mkono na wafanyabiasha wa soko la wilaya ya Ludewa.