Na John Walter-Babati
Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara imeshika namba moja kwa usafi kati ya miji 21 nchini iliyoshindanishwa na kupatiwa cheti na shilingi milioni 15.
Mwenyekiti wa halmashauri Abdulrahmani Kololi amesema hilo limewezekana kwa sababu wamewaelimisha wananchi na kukubali usafi.
Kwa ushindi huo, Halmashauri ya mji wa Babati imeifuta historia ya ushindi kwa usafi wa mazingira Halmashari ya Mji wa Njombe iliyoshika nafasi hiyo kwa miaka kadhaa mfululizo.
Akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Abdulrahmani Kololi amesema wananchi wameelewa Umuhimu wa kuwana mazingira safi ndo maana ushindi umepatikana.
Amesema kuwa Halmashauri hiyo imeweza kuwa na vyoo bora katika mitaa yake pamoja na kuwa vifaa vya kunawia mikono katika vyoo hivyo.
Kaimu mkuu wa idara ya Mazingira na Usafi Halmashauri ya mji wa Babati Aretas Laurent amesema kuwa kuna jitihada ambazo zinafanyika za kuhakisha mji unaendelea kuwa safi na kwamba hatavumiliwa mtu ambaye anachafua mazingira.
“Tutaweka vibao vya tahadhari ya kutupa taka ovyo na kutumia mgambo kuwakamata wachafuzi wa Mazingira” alisisitiza Aretas
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mjini Babati Mheshimiwa Elizabeth Marley amewataka watumishi idara ya mazingira kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa Mazingira na wasibweteke na ushindi huo.
Tukio hilo la ugawaji wa vyeti na zawadi lilifanywa na Naibu katibu Mkuu wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalaghe novemba 19,2022 Katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ikiwa ni kilele cha wiki ya usafi kitaifa na maadhimisho ya siku ya choo Duniani.