**********************
Na Victor Masangu,Pwani
Katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya Sita Mama Samia Suluhu Hassan Kikundi cha Pwani generation Qeens katika kutimiza miaka minne tangu kuanzishwa kwake kimeandaa tuzo maalumu zijulikanazo kama ‘Mwanamke Sahihi Fete’ zinazotarajia kufanyika leo ijumaa Wilayani kibaha.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kuhusiana na tafrija hiyo Mwenyekiti wa Pwani Generation Qeens Betty Msimbe(Mwanamke wa shoka) alisema kwamba maandalizi yote kwa ajili ya utoaji wa tuzo hizo za aina yake yameshakamilika na kila kinakwenda sawa.
Mwenyekiti huyo alibainisha kwamba katika tafrija hiyo kunatarajiwa kuwa na watu zaidi ya 200 kutoka maeneo mbali mbali ambao watakuja kushuhudia na kujionea utoaji wa tuzo hizo mbali mbali ambazo zitatolewa usiku wa leo katika ukumbi wa Desstin Hall eneo la kwa Mathias mjini Kibaha.
“Tunashukuru maandalizi yote mpaka Sasa yamekamilika kwa ajili ya tafrija hii ya mwanamke sahii fete kwa hiyo tutaweza kushuhudia wanawake na wanaume ambao wameweza kufanya vizuri zaidi katika kazi zao za kijasiriamali pamoja na Mambo mengine ya biashara zao,”alisema Msimbe.
Alibainisha kwamba lengo kubwa la kuandaa tuzo hizo ni kwa ajili ya kuwapa hamasa na molali zaidi wanawake na wanaume wa Mkoa wa Pwani kutumia fursa mbali mbali zilizopo katika kujipatia kipato ili kujikwamua kiuchumi.
Alibainisha katika Mkoa wa Pwani kuna wanawake wengi wamekuwa wakijitahidi katika kufanya kazi zao za kujipatia kipato na wengine ni wamekuwa na mchango mkubwa kwa jamii hivyo wakaona kuna umuhimu wa kutoa tuzo hizo ambazo zitawafanya kuwapa hamasa zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Sisi kama kikundi chetu cha Pwani Generation Qeens wanawake wa shoka tumepata usajili wetu mnamo mwaka 2019 na tumekuwa tukishiriki katika shughuli mbali mbali za kuisaidia jamii na makundi yenye uhitaji maalumu na hizi tuzo tumekuwa tukizitoa kwa walengwa wanaofanya vizuri na tutaendelea kuzifanya kila mwaka,” alifafanua Mwenyekiti huyo.
Katika hatua nyingine alisema katika tafrija hiyo pia itaenda sambamba na matukio mengine mbali mbali ikiwemo kufanya tendo la huruma kwa kutoa vifaa kwa watoto wenye ulemavu lengo ikiwa ni kuwajari na kuwathamini kama jamii nyingine.
“Pamoja na kutoa tuzo mbali mbali lakini siku ya leo pia wanawake wa shoka tutatoa vifaa kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu ya kuisaidia jamii kama mambo muhimu hasa kwa Hawa watoto wetu wenye ulemavu na pia nawahimiza watanzania wengine wawe na udhubutu wa kuchangia kwa hali na mali,”alisema.
Msimbe aliongeza kuwa katika katika tuzo hizo zitaenda sambamba na burudani kabambe za aina mbali mbali ikiwemo bendi ya Kiteshe ambayo inatikisa na kufanya vizuri katika Wilaya ya Kibaha na maeneo mingine ya Mkoa wa Pwani.
Tuzo za Mwanamke sahihi Fete 2022 mwanamke wa shoka Mkoa wa Pwani zimedhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini,Silvestry Koka,Tim Cocktail,Flo designs,Smart studio,Apexdesign,Destiny hall,Kiteshe lodge &pub,Mc akida,Anne stationary,pamoja na Betty’s liQuor store.