Jeshi la Paolisi Mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa ya kupatikana kwa mwili wa askofu mstaafu wa kanisa la Aglikana Diocese ya Victoria Nyanza, Boniphace William@Kwangu, Miaka 61, Mkazi wa Shibula, wilayani Ilemela, aliyekutwa amefariki na mwili wake ukielea ndani ya maji kando ya ziwa victoria karibu na eneo linapojengwa daraja la Dr. John Pombe Magufuli (JPM).
Ni kwamba, tarehe 28.11.2022 majira ya asubuhi huko Shibula Wilaya ya Ilemela Boniphace William@Kwangu aliaga familia yake na kuelekea wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kupokea malipo ya mwisho ya shilingi 2,500,000/= baada ya kuwa ameuza eneo lake pamoja na nyumba kwa kanisa la KKKT- Sengerema. Hata hivyo hakuweza kulipwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa wanunuzi walimtaka awasilishe nyaraka ya umiliki wa eneo hilo hivyo, alirudi Mwanza mjini kwa ajili ya kushughulikia nyaraka hizo.
Kwamba, ilipofika jioni ya siku hiyo familia yake walipata wasiwasi kuhusu alipo Boniphace William@Kwangu kwani hakuwa amerudi nyumbani pia alikuwa hapatikani kwenye simu yake ya mkononi. Kutokana na hali hiyo ilibidi familia yake watoe taarifa Kituo cha Polisi Kirumba.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na familia na watu mbalimbali lilianza kufanya ufuatiliaji ili kubaini alipo askofu huyo mstaafu. Wakati uchunguzi ukiendelea tarehe 01.12.2022 majira ya 10:00 jioni zilipatikana taarifa kutoka kwa wananchi wema kwamba, huko katika kijiji cha Kigongo, kata ya Idetemya wilaya ya Misungwi ndani ya maji katika ziwa victoria jirani na daraja la Dr. John Pombe Magufuli umeonekena mwili wa mtu wa jinsia ya kiume ukiwa unaelea majini. Baada ya askari kwa kushirikiana na wananchi kuopoa mwili huo ulitambulika kuwa ni wa Boniphace William@Kwangu.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali kwa hatua za kiuchunguzi kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo hivyo tunaiomba familia, ndugu, jamaa na wananchi kwa ujumla wenye taarifa zozote kuhusiana na tukio hili wazitoe kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi.
Imetolewa na:-
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza
S.L.P 120,
Mwanza.