Mwaklishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Mkoa wa Ruvuma ambayo kimkoa yamefanyika Kata ya Luwaita wilayani Mbinga
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Aziza Mangosongo akikagua mabanda kwenye viwanja cha Luwaita wilayani Mbinga ambako yalifanyika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani kimkoa
******************
MKOA wa Ruvuma kwa mwaka 2022 unakadiriwa kuwa na zaidi ya watu 63,088 wanaoshi na Virusi vya UKIMWI.
Haya yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Lous Chomboko wakati anatoa taarifa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo kimkoa yamefanyika Kata ya Luwaita wilayani Mbinga.
Dr.Chomboko amebainisha kuwa kati ya watu hao wanawake ni 37,233,wanaume ni 22,849 na Watoto ni 3,008.
“Kaulimbinu ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba Mosi ni Imarisha usawa,kauli hii imelenga usawa katika ngazi za familia kwa kutokuwatenga watu wanaopata maambukizi’’,alisisitiza Dr.Chomboko.
Mganga Mkuu wa Mkoa ameutaja Mkoa wa Ruvuma kuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI kipo juu zaidi ya kiwango cha kitaifa.
Amesema kiwango cha maambukizi ya VVU na UKIMWI mkoani Ruvuma ni asilimia 5.6 ambapo kiwango cha kitaifa ni asilimia ni asilimia 4.7.
Hata hivyo amesema kiwango hicho cha maambukizi kimkoa kimepungua kwa asilimia 1.4 kutoka asilimia saba hadi 5.6 kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI na malaria kwa mwaka 2011 hadi 2012.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani,Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Aziza Mangosongo,amesisitiza jamii nzima kuwajali watu wenye VVU na UKIMWI.
Amesema licha ya jitihada zote za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI hali ya maambukizi katika Mkoa wa Ruvuma sio nzuri kwa sababu kiwango cha maambukizi kimkoa ni kikubwa zaidi ya kiwango cha maambukizi kitaifa.
“Hivyo basi inatulazimu kuendelea kujikumbusha juu ya mikakati ya mapambano dhidi ya UKIMWI ili kuendelea kupunguza maambukizi ya VVU katika Mkoa wetu’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bakari Mketo amewapongeza wadau wa afya mkoani Ruvuma kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali zinazosaidia kupunguza maambukizi mapya ya VVU ikiwemo tohara na uhamasishaji wa kupima VVU hali iliyosababisha asilimia 98.8 ya watu wanaoishi na VVU mkoani Ruvuma kujua hali zao.