Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu leo Desemba Mosi, kulia kwake ni Mkuu wa TaSUBa, Dkt. Herbert Makoye.
Wahitimu wa ngazi za stashahada na astashahada katika kozi za Sanaa za maonesho, Picha jongefu na uzalishaji wa muziki na sauti wakiwa katika maandamano kuelekea katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) yalipofanyika mahafali ya 33 ya taasisi hiyo leo Desemba Mosi, 2022 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani
Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akitoa hotuba yake.
Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye akitoa hotuba yake wakati wa mahafali ya 33 ya taasisi hiyo yaliyofanyika leo Desemba Mosi, 2022 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Bw. George Yambesi akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya taasisi hiyo ambayo yamefanyika leo Desemba Mosi, 2022 katika kampasi ya TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani. Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul Muhitimu Richard Julius Mtambo akisoma risala iliyoandaliwa na wahitimu wakati wa mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambayo yamefanyika Desemba Mosi, 2022 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo leo Desemba Mosi, 2022. Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akipitishwa kujionea bunifu mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa taasisi hiyo leo Desemba Mosi, 2022.
Vikundi vya burudani ambao ni wanafunzi wa TaSUBa wakitoa burudani mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul wakati wa mahafali ya 33 ya TaSUBa yaliyofanyika leo Desemba Mosi, 2022 katika kampasi ya TaSUBa, Bagamoyo mkoani Pwani.
Wahitimu wa ngazi za stashahada na astashahada katika tasnia za sanaa na utamaduni.
**************
Na Mwandishi Wetu Bagamoyo
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Sanaa na utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa usimamizi mzuri wa fedha zinazoletwa katika taasisi hiyo kwa kuzitumia vyema kuendana na mahitaji ya taasisi ili kuifanya taasisi kufikia malengo yake.
Mbali na hilo, pia ameipongeza TaSUBa kwa ongezeko kubwa la udahili wa Wanafunzi katika chuo hicho hata kufikia hatua ya kuweka historia ya kudahili idadi kubwa ya wanafunzi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Naibu Waziri Gekul ametoa pongezi hizo leo Desemba Mosi, 2022 akiwa ni mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya TaSUBa yaliyofanyika katika kampasi ya TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani na kusisitiza kuwa, taaluma ya utamaduni na sanaa inayotolewa chuoni hapo ni taaluma muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote duniani.
Kufuatia hilo naibu waziri Gekul amebainisha kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona wazi umuhimu wa taaluma hiyo na hivyo kuanzisha sera maalum kusimamia.
“Taaluma inayotolewa hapa chuoni ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote duniani, ndio maana serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, imeweka sera ya kusimamia sanaa na utamaduni kwa ujumla wake” alisema Naibu Waziri Gekul na kuongeza
“TaSUBa ni taasisi ya pekee nchini kwetu na ukanda wa Afrika Mashariki inayotoa mafunzo ya sanaa kwa ngazi ya stashahada na astashahada hivyo basi kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha taaluma hii ili iendane na mazingira ya sasa ya utandawazi”
Naibu Waziri huyo ameutaka uongozi wa TaSUBa kuendeleza ubunifu zaidi kwa kuanzisha kozi ambazo zitawavutia watu wengi kujiunga na chuo hicho.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye amesema kuwa, kwa miaka mitatu mfululizo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi chuoni hapo na hiyo ni kutokana na jitihada mbalimbali zilizochuliwa na serikali ya awamu ya sita, wadau pamoja na wao wenyewe kama taasisi.
Dkt. Makoye amezitaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uamuzi wa serikali kuwapangia wahitimu wa kidato cha nne moja kwa moja kujiunga na chuo hicho pamoja na uhamishaji wa kila siku unaofanywa na TaSUBa pamoja na wadau wengine katika kukitangaza chuo hiko.
Dkt. Makoye ameongeza kuwa, kwa mwaka huu wa masomo pekee wameweka kudahili wanafunzi 835 kutoka kwenye lengo la kudahili wanafunzi 700 na hivyo kuweka historia ya udahili mkubwa chuoni hapo.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la wahitimu na kwa mwaka huu tuna wahitimu 217. Aidha, mwaka huu wa masomo 2022 /2023 tumeweza kudahili wanafunzi 835, lengo lilikuwa ni kudahili wanafunzi 700. Hii ni rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa TaSUBa” alisema Dkt. Makoye
Kuhusu maono ya TaSUBa kumiliki kituo chake cha redio na televisheni kwa ajili ya kuwezesha wepesi wa utendaji kazi na mazingira wezeshi ya ufundishaji na kujifunza Dkt. Makoye amesema.
“Endapo tukipata fedha ambazo tuliziomba katika mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ununuzi wa vifaa vya kuanzisha na kusimika mitambo ya televisheni na redio, basi TaSUBa itakwenda kumiliki televisheni na redio yake”
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TaSUBa, Bw. George Yambesi ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika taasisi hiyo unalenga kupanua wigo zaidi wa vijana wa Kitanzania kupata mafunzo katika tasnia za sanaa na utamaduni.
Aidha, Bw. Yambesi ametumia fursa hiyo, kuishukuru serikali kwa uwezeshaji mkubwa unaoendelea kutolewa kwa TaSUBa, uwezeshaji ambao umeleta matokeo chanya katika taasisi hiyo ikiwemo kufanikisha uboreshaji wa miundombinu kujifunzia na kufundishia kinyume na iliyokuwa awali ambao pia ameendelea kuisihi serikali kuendelea na uwezeshaji huo ili malengo mahususi yaliyowekwa na TaSUBa yaweze kutimiza na taasisi hiyo iweze kuleta tija kw mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.
Nao wahitimu wa chuo hicho kupitia risala yao iliyosomwa na Richard Julius Mtambo wameeleza kuwa changamoto kubwa mbili zinazowakabili chuoni hapo ni ukosefu wa basi la taasisi na hivyo kupata adha kubwa pale wanapopanga kufanya safari za kimasomo, utalii, maonesho, mafunzo, mashindano na za kikazi.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa uzio kwenye taasisi hiyo jambo ambalo linahatarisha usalama, kuwa kichocheo cha wizi na kupelekea kukosekana kwa faragha.
Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni kituo chenye ubora uliotukuka Afrika Mashariki katika kutoa mafunzo ya sanaa za maonesho na ufundi ambapo majukumu yake makubwa ni kuhudumia mahitaji ya nchi washirika wa jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutunza, kuhamasisha na kuendeleza sanaa za maonyesho na ufundi ikiwa na majukumu makuu matatu ambayo ni utoa mafunzo,
kufanya utafiti katika masuala yanayohusu sanaa na utamaduni pamoja na kutoa ushauri katika masuala yanayohusu sanaa na utamaduni.