Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WIZARA ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imewataka Maofisa biashara wote nchini kusimamia taaluma zao katika utekelezaji wa majukumu yao lengo likiwa kuwa mfano bora wa uwezeshaji wa biashara kwenye mamlaka za serikali za mitaa.
Pia wizara hiyo imesema kwa kushirikiana na taasisi 17 zilizochininya Kurugenzi ya maendeleo ya biashara wanatekeleza lengo kuu la kuwezesha biashara Kwa kuwatumia maofisa biashara wanawake.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi idara ya maendeleo ya biashara katika wizara hiyo Christopher mramba, kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo DK.Ashantu Kijani wakati wa uzinduzi wa Chama cha Maofisa Biashara wanawake(TAWTO).
Mramba amewasii Maofisa hao katika utekelezaji wa majukumu yao wahakikishe wanakuwa wawekezaji wa biashara na si wakwamishaji, kutoa elimu na kuwasaidia wafanyabiashara kujitambua nini wanapaswa kufanya ili kukuza na kuboresha biashara zao.
Alisema katika kutekeleza lengo kuu kuwezesha biashara wanawatumia maofisa biashara wanawake kutoka taasisi za Kwa kushirikiana na maofisa biashara waliopo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) katika Halmashauri zote nchini ili kutengeneza Mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Awali akiwasilisha taarifa mwenyekiti wa chama Elizabeth Swagi amesema licha ya uwepo juhudi kadhaa kwa upande wa Serikali na sekta binafsi katika kuwasaidia wanawake wafanyabishara, bado wanakumbana na changamoto mbalimbali hasa katika sekta isiyo rasmi.
Mwenyekiti huyo amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na Kiwango kidogo cha elimu kuhusu biashara,Taratibu ndefu au urasimu katika kuanzisha biashara, Kutokuwa na mtaji wa kutosha, Kukosekana kwa mikopo yenye riba nafuu, Kunyimwa haki ya kumiliki mali, hivyo kukosa dhamana ya mikopo.
Changamoto nyingine ni “Sheria na kanuni kulenga zaidi makampuni makubwa na kusahau wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati na Unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo ukatili wa kingono unaofanywa na baadhi ya maafisa kwenye sekta ya biashara,”amesema Elizabeth.
Ameyataja mafanikio yaliyopatikana ndani chama hicho kuwa ni pamoja na kupata usajili wa kudumu kutoka Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, kwa cheti Namba S.A.22943Usajili wawanachama hai Hamsini na saba (57) toka Mikoa yote ya Tanzania Bara.
“Tumefanikiwa kufungua Akaunti Namba 50510086481 Yenye jina Tanzania Women Trade Officers katika Benki ya NMBKuendesha Mikutano miwili ya chama kwa gharama za chama,” amesema Mwenyekiti huyo.
Pia Chama hicho kiliomba, Wizara ziweze kuwaruhusu na kuwawezesha wanachama wao kuweza kushiriki mikutano mbalimbali inayoandaliwa na chama na pia kutokana na uchanga wa chama wanaomba Wizara ya Uwekezaji na Ofisi ya Rais TAMISEMI ziwawezeshe kuchangia gharama za uendeshaji wa Mikutano ya Mwaka kadiri ya kalenda ya chama.
Naye Katibu wa Chama hicho, Bertha George amesema wameamua kuwa na chama hicho Kwa wakati huu kutokana na utandawazi, hivyo wanalazimika kwenda sambamba na Karne ya sayansi na Teknolojia ili kuweza kutoa elimu kisasa na kuibua fursa zaidi za kibiashara ndani na nje ya nchi.