***************
Kamati ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Committee) ilikutana tarehe 28 Novemba
2022 ambapo ilifanya tathmini ya utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa
uchumi.
Kutokana na tathmini hiyo, na kwa kuzingatia athari za mtikisiko wa uchumi
duniani kwenye mfumuko wa bei na shughuli za uchumi, Kamati iliridhia Benki Kuu
iendelee na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi
katika uchumi kwa mwezi Novemba na Desemba, 2022.
Utekelezaji huu wa sera ya fedha unalenga kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unaendelea kubakia ndani ya lengo na kuwezesha ukuaji wa uchumi nchini. Aidha, uamuzi huo unalenga kufikia malengo ya sera ya fedha ya robo ya mwaka inayoishia mwezi Desemba 2022.
Kamati pia ilijadili mwenendo wa uchumi wa dunia na kubaini kuwa bado
umeendelea kutoridhisha, hali ambayo imepelekea Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
kushusha makadirio ya ukuaji wake kwa mwaka 2022 na mwaka 2023, ikilinganishwa
na makadirio ya awali.
Mfumuko wa bei umeendelea kuwa juu ya malengo katika nchi
nyingi kutokana na ongezeko la bei za bidhaa na mabadiliko ya hali ya hewa, na
kupelekea benki kuu kuchukua hatua za kupunguza ukwasi ili kukabiliana na
changamoto hiyo.
Vilevile, Kamati ilijadili na kuridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo
wa uchumi nchini kwa kipindi cha hivi karibuni, licha ya kukabiliana na changamoto
zilizotokana na mwenendo wa uchumi wa dunia. Kamati ilibainisha kuwa:
i. utekelezaji wa sera ya fedha uliendana na malengo yaliyowekwa na
matokeo yake yalikuwa ya kuridhisha. Kiwango cha ukwasi katika sekta ya
benki kilikuwa cha kutosha na ulikuwa sawia na lengo la kudhibiti
ongezeko la mfumuko wa bei. Aidha, malengo ya sera ya fedha kwa mwezi
Septemba 2022 yaliweza kufikiwa;
ii. mwenendo wa uchumi nchini ulikuwa wa kuridhisha, ambapo kwa
Tanzania Bara uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2022. Hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa
makadirio ya ukuaji wa asilimia 4.7 kwa mwaka 2022. Kwa upande wa
Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 5, sawia na makadirio ya ukuaji wa
asilimia 5.4 kwa mwaka 2022. Ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuendelea
kuimarika, kufuatia kuanza kupungua kwa athari zinazotokana na mtikisiko
wa uchumi duniani;
iii. mfumuko wa bei umeendelea kuwa wa wastani, japokuwa umekuwa
ukiongezeka kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na nishati. Kwa
upande wa Tanzania Bara, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 4.9 kwa mwezi
Oktoba 2022 kutoka asilimia 3.8 mwezi Julai 2021, kiwango ambacho bado
kilikuwa chini ya lengo la asilimia 5.4 kwa kwaka 2022/23.
Kwa upande wa Zanzibar mfumuko wa bei umefikia asilimia 7.3 kutoka asilimia 2.2,
ikilinganishwa na lengo la asilimia 5. Mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia
ndani ya malengo katika kipindi kilichosalia kwa mwaka 2022/23;
iv. ujazi wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi umeendelea kuongezeka kwa
kiwango cha kuridhisha. Ujazi wa fedha ulikua kwa asilimia 13.4 mwezi
Oktoba 2022, sawia na lengo la ukuaji wa asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23.
Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa kasi zaidi, kufikia asilimia 22 na
asilimia 23.7 mwezi Septemba na Oktoba 2022, mtawalia, ikilinganishwa na
lengo la asilimia 10.7 kwa mwaka 2022/23;
v. mapato ya Serikali katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 yalikuwa
ndani ya malengo. Kwa upande wa Tanzania Bara, mapato yalifikia asilimia
96 ya lengo, wakati kwa Zanzibar yalikuwa asilimia 98.5 ya lengo.
Matumizi
yalifanyika kuendana na malengo na kwa kuzingatia umuhimu wa
kukabiliana na madhara yatokanayo na athari za mtikisiko wa uchumi wa
dunia, pamoja na kugharamia ujenzi wa miundombinu;
vi. sekta ya nje imeendelea kuwa thabiti na tulivu, licha ya changamoto
zinazotokana na athari za uchumi wa dunia. Akiba ya fedha za kigeni
iliendelea kuwa imara, kiasi cha kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya
nchi kwa kipindi cha miezi 4.2.
Kiwango hicho kilikuwa juu ya lengo la nchi
la kutosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi minne. Kiwango
cha utoshelevu wa fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa na huduma kutoka
nje kinatarajiwa kuongezeka kutokana na kuendelea kupungua kwa bei za
bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hususan bei ya mafuta; na
vii. mwenendo wa sekta ya benki ulikuwa wa kuridhisha, ukiwa na ukwasi wa
kutosha kuendana na mahitaji ya shughuli mbalimbali za kiuchumi, pamoja
na mtaji kulingana na misingi ya sheria na kanuni na yenye kutengeneza
faida.
Vilevile, sekta imekuwa na ongezeko la rasilimali na amana,
sambamba na kuongezeka kwa ubora wa mikopo kwa ujumla.
Katika
kipindi kinachoishia mwezi Oktoba 2022, kiwango cha mikopo chechefu
kilipungua na kufikia asimia 7.2 ya mikopo yote kutoka asilimia 8.3 katika
kipindi kama hicho mwaka 2021.
Gavan