Chujio la maji linaloendelea kujengwa katika mradi wa Igando Kijombe wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo wa kwanza kushoto na Meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Mhandisi Sadick Sakka wa pili kushoto wakiangalia sehemu ya miundombinu ya mradi wa maji unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 11.4 wilayani Wanging’ombe.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Ruwasa Mhandisi Ndele Mengo kushoto,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo baada ya kukagua mradi wa maji wa Igando-Kijombe wilayani Wanging’ombe unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 12.4 ambapo Kivegalo amemtaka Mkurugenzi huyo wa Ufundi kupiga kambi katika mradi huo hadi utakapokamilika.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,akizungumza na wataalam kutoka Ruwasa makao makuu na mkoa wa Njombe baada ya kukagua mradi mkubwa wa maji wa Igando-Kijombe mkoani Njombe ulioanza kutekelezwa mwaka 2018 na Kampuni ya STC Contruction Company Ltd kwa gharama ya Sh.bilioni 12.4 ambao hadi sasa bado haujakamilika.
Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo kulia,akizungumza na mwakilishi wa Kampuni ya STC Contruction Company Ltd inayojenga mradi wa maji wa Igando-Kijombe ambaye hakufahamika jina lake baada ya kukagua mradi huo ambao uko nyuma kwa miaka mitatu ya utekelezaji wake.
Picha na Muhidin Amri
……………………………….
Na Muhidin Amri,
Wanging’ombe
MKURUGENZI mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijiji(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo,amemuagiza Mkurugenzi wa ufundi wa Ruwasa Mhandisi Ndele Mengo,kupiga kambi na kusimamia mradi wa maji Igando-Kijombe wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe hadi utakapo kamilika.
Kivegalo,ametoa mwezi mmoja kwa kampuni ya STC Contruction Ltd inayojenga mradi huo kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Kivegalo,amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kutoridhishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa mradi huo unaotekezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 12,437,407,360 lakini bado haujakamilika tangu mwaka 2018.
Amemtaka mkandarasi kufanya kazi kwa weledi ,na kuachana na mambo ya ovyo yanayoweza kupelekea mradi kujengwa chini ya kiwango na kusababisha wananchi kuchelewa kupata huduma ya maji.
Aidha,amemshauri kuongeza idadi ya vibarua watakao fanya kazi usiku na mchana ili kazi ikamilike haraka na wananchi waanze kupata huduma ya maji katika maeneo kwa kuwa wamechoka kusubiri kwa muda mrefu.
Kivegalo,amemuagiza meneja wa Ruwasa wilaya ya Wanging,ombe Charles Mengo na Meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Sadick Chakka kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo ili aweze kurekebisha kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza na wahakikishe kazi zote zilizopangwa kutekelezwa zinafanyika kwa ubora wa hali ya juu.
Alisema,Serikali imewaamini wataalam wa Ruwasa katika kusimamia miradi ya maji,hivyo ni jukumu la kila mmoja kumsaidia kazi Rais Samia Suluhu Hassan kufanikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
“ni lazima sisi kama wataalam tuitendee haki serikali yetu kwa kujenga na kusimamia miradi yote ya maji kwa ubora wa hali ya juu,licha ya kuwepo kwa wakandarasi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao”alisema Kivegalo.
Mradi wa maji Igando-Kijombe ulianza kutekelezwa mwezi Oktoba mwaka 2018 na ulitakiwa kukamilika mwaka 2019 kabla ya Ruwasa kukabidhiwa mradi huo,hata hivyo bado haujakamilika na uko nyuma kwa mujibu wa mkataba.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilaya ya Wanging’ombe Charles Mengo alisema, mradi huo ulikabidhiwa kwa Ruwasa mwezi Disemba 2019 kutoka Halmashauri ya wilaya huku utekelezaji wake ukifikia asilimia 13.
Alisema, kwa sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 86 na thamani ya kazi zilizotekelezwa ni Sh.bilioni 8.140396394.16 ambazo zimetumika kumlipa mkandarasi kwa awamu tofauti.
Naye mwakilishi wa kampuni ya STC Contruction Ltd Jamal Hamis amehaidi kukamilisha kazi kabla ya tarehe 31 Disemba kwa kuwa ndani ya wiki moja vifaa vyote vya kazi vitakuwa vimefika eneo la mradi.