Meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete mkoani Njombe Mhandisi Innocent Lyamuya,akitoa taarufa ya utoaji huduma ya maji na hali ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Utweve kata ya Ukwama wilayani humo unaotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa gharama ya zaidi ya Sh,milioni 300.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Utweve na watumishi wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Makete mkoani Njombe,wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo kushoto aliyetembelea mradi wa maji unaojengwa katika kijiji hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo akishuka kwenye ngazi baada ya kukagua ujenzi wa tenki la maji linalojengwa kwa ajili ya kuhudumia zaidi ya wakazi 1,400 wa kijiji cha Utweve wilayani Makete.
***********************
Na Muhidin Amri,
Makete
MKURUGENZI mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo,amewataka wataalam wa maji kufanya kazi kwa kujituma na kutimiza wajibu wao na kuhakikisha wanaondoa changamoto za upatikanaji wa huduma za maji kwa wananchi badala ya kusubiri maagizo ya viongozi.
Alisema,tabia ya kusubiri maagizo na maelekezo kutoka kwa viongozi wa ngazi ya juu imeshapitwa na wakati, badala yake kila mmoja anatakiwa kuwajibika na kutekeleza majukumu katika eneo lake.
Kivegalo ameyasema hayo jana,mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa katika kijiji cha Utweve kata ya Ukwama wilayani Makate kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 300.
Amewataka,wataalam hao kutumia weledi na taaluma zao kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea,kwani tabia hiyo inaweza kuchelewesha lengo la serikali kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 maeneo ya vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.
“ sio vizuri kusubiri hadi maagizo ya viongozi,tunatakiwa tuwe mbele ya wananchi na viongozi na lazima tuandae program(mipango) ya kazi zetu na bahati nzuri kijiji hiki ndicho alichozaliwa Katibu Mkuu wa wizaya ya maji Antony Sanga,hivyo ni lazima tumtendee haki kwa kufanya vizuri kwenye miradi ya maji”alisema.
Katika hatua nyingine Kivegalo,amempongeza meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete Innocent Lyamuya kwa matumizi mazuri ya fedha zilizoletwa kutekeleza mradi huo,kwani fedha zilitumika ni kidogo huku ujenzi wa mradi umefikia zaidi ya asilimia 70.
Alisema,miaka ya zamani mradi kama huo ulitumia zaidi ya Sh.milioni 800 na zaidi,lakini Ruwasa wilaya ya Makete imetumia kiasi kidogo huku tayari baadhi ya maeneo katika kijiji hicho wananchi wameanza kupata huduma ya maji.
Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete Innocent Lyamuya alieleza kuwa,hadi sasa fedha zilizopokelewa ni Sh.milioni 293,653,651 na zilizotumika ni Sh.milioni 216,860 na fedha zilizobaki ni Sh.milioni 11.2.
Aidha Lyamuya alisema,mradi huo utakapo kamilika utahudumia wakazi 1,400 wakiwamo wanafunzi 600 wa shule ya Sekondari ya Wasichana Makete.
Aliongeza kuwa,hadi sasa baadhi ya kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo vimekamilika ikiwamo ujenzi wa vituo 8 kati ya 15 vya kuchotea maji na wananchi wameanza kupata huduma ya maji katika maeneo yao.
Diwani wa kata ya Ukwama Emmanuel Sanga alieleza kuwa,katika kijiji cha Utweve changamoto ya maji ilikuwa kubwa na ya muda mrefu,hivyo kusababisha shughuli za kiuchumi kwenda taratibu na wanafunzi kuacha masomo na kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Utweve,wameishukuru serikali kupitia Ruwasa kujenga mradi huo ambao umewezesha kumaliza changamoto ya huduma ya maji katika kijiji hicho.
Daynes Sanga alisema,kabla ya mradi huo walilazimika kutumia maji ya visima na vyanzo vingine vya asili kwa kupata maji kwa matumizi,hata hivyo ameomba waruhusiwe kutumia maji hayo kuanzisha bustani ndogo ndogo za mboga.
Fedisia Sanga alisema,kwa muda mrefu walikuwa wanatumia maji kutoka kwenye visima vya asili ambavyo wakati wa kiangazi havikutoshelezi kutokana na mahitaji makubwa na wakati mwingine kukauka.