Na John Walter-Manyara
Wakazi wa mtaa wa Kiongozi kata ya Maisaka wilayani Babati mkoani Manyara, leo wameandamana kuifunga barabara kuu ya Babati-Arusha, wakishinikiza kuwekwa tuta katika bara bara hiyo baada ya kugongwa mwanafunzi na kufariki dunia akivuka Kuelekea shuleni.
Mwanafunzi huyo wa kike wa shule ya msingi Kiongozi alifariki dunia papo hapo.
Tukio hilo lililotokea leo Novemba 28,2022, limesababisha usafiri wa magari ya abiria kusimama katika barabara hiyo na kuzua tafrani kubwa kuanzia majira ya saa mbili asubuhi hadi saa tano asubuhi walipofika viongozi wa wilaya na polisi.
Akizungumza katika eneo hilo la , Mwenyekiti wa mtaa wa Kiongozi Thomas Duwe, alisema wananchi wa eneo hilo wamechoshwa na kwamba awali tuta lilikuwepo na kuondolewa bila kujua sababu.
“Hatuwezi kuvumilia watu kugongwa kutokana na barabara hii, kukosa tuta na kivuko,yaani mpaka watoto watumbukie kwenye mtaro ndo waweze kuvuka,tumechoka ”walisema kwa nyakati tofauti.
Wakazi wa eneo hilo waliokuwa barabarani hapo, walisema sio Mara ya kwanza kutokea tukio la watoto kugongwa, hivyo ni bora barabara waifunge ili kuepusha maafa zaidi.
Baada ya majadiliano baina ya wananchi, Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange na viongozi wa mtaa huo, hatimaye wananchi walikubali kutoa Majani waliyoweka barabarani na barabara kupitika.
Mkuu huyo wa wilaya Lazaro Twange aliyekuwa na Wataalamu kutoka TANROADS Manyara, ameeleza eneo hilo litawekewa tuta na kivuko kuanzia kesho Novemba 29,2022.