******************
Na Mwandishi Wetu,
MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashekhe ya Maadili Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga amewakemea vikali wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao kutwa nzima wanazurura kutafuta vyeo baadala ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutatua kero za Watanzania.
Askofu Mwamalanga ametoa karipio hilo, wakati akizungumza na wakina mama 100 wa CCM walionde kuombewa dua, ili uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) unaofanyika kesho ufanyike kwa amani na salama.
Mwamalanga alisema matamanio yake ilikuwa kuona wana CCM wanakuwa bize kumsaidia Rais Samia kwa kusimamia maagizo yake kila siku, lakini anachokiona wapo bize kutafuta dua za kupata uongozi na wengine wanatafuta kuwa Rais Samia baada ya mwaka 2025.
“Jamani mbona hivyo, msaidieni Rais Samia kuhudumia wananchi mnamchosha, jifunzeni kwetu viongozi wa dini kutwa tunamuombea dua njema, lakini hatuishii kuomba tuu tunawasaidia Watanzania kwa kuchimba visima vya maji kupanda miti na kuelimisha wananchi kutunza misitu ya asili ukiuliza Askofu ni nani hapa bara na visiwani kule kwa Mheshimu Dk Hussein Ally Mwinyi, wananiita yule bwana mazingira kwa sababu kuhimiza upandaji miti.
Ukifika kule Mbeya mjini watakuambia miti yote hiyo ni bwana mazingira Askofu Mwamalanga, lakini tupo pia bega kwa bega na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kupambana na uingizaji wa dawa ya kulevya, ili kutimiza hitaji laTanzania bila dawa za kulevya inawezekana,” alisema.
Askofu huyo alisema wana CCM waliowengi wamejikita kumteta Rais Samia mara kile mara lile na kusaka madaraka tena kwa rushwa.
“Juzi Rais Samia amesema jambo la maana mno juu ya haki za Watanzania zinazokiukwa kwa sababu ya ubambikizwaji wa kesi kwa wanyonge. Leo CCM hamlisemi Mh Samia amewambia wanasheria madhara ya kuwabambikia watu kesi kunavyojaza magerezani na kupunguza nguvu kazi ya nchi.
Nilitegemea wanawake wa CCM mnahamasisha Watanzania kupenda haki kwa maandamano, lakini ninyi kutwa kutafuta vyeo ambavyo havitokani na haki ,”alisisitiza.
Askofu Mwamalanga alisema amesikitishwa na baadhi ya viongozi wa CCM kutwa wanajitahidi kujenga chuki kwa wananchi ili Rais Samia achukiwe na kwamba hiyo siyo sahihi hata kidogo ila ni kukosa ustaarabu.
Alisema Rais Samia ana dhamira njema ya kufikia ustawi wa pamoja na hataki kubagua watu kama baadhi yao wanavyopendelea.
Mwamalanga alisema Tanzania hatuna makaburu wakandamizaji na wakandamizwaji, ila bado CCM kuna watu wadumavu wa mawazo na akili ambao wanapenda viongozi wote wa vyama vingine wawe wanakamatwa na kuwekwa jela na hata kuuwaawa hiii ni hatari mno kwa watu wa jinsi hii.
Alisema kundi hilo likiona Rais Samia anatenda haki wanachukia, hivyo amewashauri waondokane na dhana hiyo na waende kuwa wajumbe sahihi.
“Tunauombea uchaguzi wa UWT uwe wa amani na furaha, wapatikane viongozi watakao msaiidia Rais Samia kuongoza Watanzania wote kula milo minne kwa siku siyo nusu mlo wa sasa …
Leo hii wakulima wa kahawa mkoani Songwe, Wilaya ya Mbozi hawajalipwa fedha zao za kahawa tangu mwezi juni mwaka huu walipouza.
Nendeni mkamwambie Rais hilo, pia mkamwambia figisu figisu za kule Mbarali ambapo maelfu ya wakulima wa mpunga wanafukuzwa kwenye ardhi yao kwa kizingizio cha uhalibifu wa mazingira,” alisema.
Askofu aliwataka wakina mama hao wakamwambieni Rais anadanganywa na anachonganishwa na Watanzania.