Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia EZEKIA EMMANUEL LUHWESHA (31) Mchimbaji na Mnunuzi wa Madini, Mkazi wa Matundasi Wilaya ya Chunya kwa tuhuma za mauaji ya wakala wa maegesho ya magari aitwaye WILLIAM MGAYA (58) Mkazi wa Mama John Jijini Mbeya.
Ni kwamba mnamo Novemba 26, 2022 majira ya saa 04:30 asubuhi huko maeneo ya Mafiati ofisi ya TARURA katika jengo la TAFISA lililopo Kata ya Ruanda, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya, WILLIAM MGAYA akiwa na mwenzake aitwaye ALMAS OMARY SHABAN (32) wote ni mawakala wa maegesho ya magari halmashauri ya Jiji la Mbeya wakiwa katika kazi yao ya kukusanya ushuru unaotokana na kuegesha vyombo vya moto walimkamata mtuhumiwa EZEKIA EMMANUEL LUHWESHA baada ya ku scan namba yake ya Gari T.772 DVY Toyota Hilux na kugundua kuwa Gari hilo lina deni la Tshs.7,500/=.
Mtuhumiwa alitakiwa kulipa deni hilo lakini alihitaji kuona hilo deni linatokana na maegesho gani hivyo kulazimika kuongozana naye hadi zilipo ofisi za TARURA kwa ajili kuangalia kwenye mfumo ili kupata taarifa za deni hilo. Mtuhumiwa alionyeshwa taarifa za deni hilo na kuridhika kuahidi kulipa deni hilo lakini wakala WILLIAM MGAYA alimtaka kulipa deni hilo papo hapo kutokana na deni hilo kuwa la muda mrefu ndipo yalitokea majibizano kati ya marehemu na mtuhumiwa hali iliyopelekea mtuhumiwa kutoa silaha yake Pistol na kufyetua risasi moja uelekeo alipokuwa WILLIAM MGAYA na kumpiga sehemu ya kifuani upande wa kulia na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.
Mtuhumiwa pamoja na Silaha Pistol aina ya Tisasi yenye namba T.0620-19J0037 ya mtuhumiwa ikiwa na risasi 09 ndani ya magazine anashikiliwa na Jeshi la Polisi.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga ACP anatoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa za malalamiko yao au kitendo chochote wanachofanyiwa kinyume cha sheria au taratibu zilizopo kwa viongozi wa mamlaka husika kwa ajili ya ufuatiliaji na hatua zaidi za kisheria.
Aidha Kamanda Kuzaga anatoa wito kwa wale wote wanaomiliki silaha kuzingatia masharti ya umilikishwaji wa silaha hizo pamoja na kuhakikisha silaha hizo wanazitumia kulingana na hitaji/mahitaji ya msingi waliyoombea silaha hizo na sio kutishia ama kuua watu jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na masharti ya umiliki wa silaha.
Imetolewa na:
ACP Benjamin E. Kuzaga
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.